Kuidhinishwa rasimu ya uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) hatimaye limeipigia kura ya ndio rasimu ya uanachama kamili wa Palestina katika umoja huo baada ya Marekani kukwamisha suala hilo kwa miaka kadhaa.
Mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu azimio la kuimarisha haki na mafao mengine ya Palestina, ambalo linalitaka Baraza la Usalama kupitia upya ombi la Palestina la kuwa mwanachama wa 194 wa Umoja wa Mataifa, ulifanyika Ijumaa asubuhi katika makao makuu ya taasisi hiyo mjini New York. Rasimu ya azimio la kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo imepasishwa kwa kura 142 za ndio, 9 za hapana na nchi 25 zikijizuia kupiga kura inaipatia Palestina haki na mafao zaidi katika Umoja wa Mataifa. Kwa sasa Palestina ni mtazamaji asiye mwanachama, lakini imekuwa ikijaribu kuwa mwanachama kamili wa taasisi hiyo ya kimataifa kwa miaka mingi. Jitihada hizi zimepingwa mara kadhaa na Marekani ambapo mwezi Aprili iliipiga veto rasimu hiyo katika Baraza la Usalama la UN.
Ingawa, kwa kuzingatia azimio hilo, Palestina itapewa haki na nafasi zaidi, kama vile kujiunga na mashirika na taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa, lakini kuna njia ndefu kabla ya Palestina kuwa mwanachama kamili wa taasisi hiyo muhimu ya kimataifa. Hata hivyo, juhudi za jamii ya kimataifa za kutambua haki na malengo ya taifa la Palestina wakati huu ambapo wananchi wa ardhi hiyo wanakabiliwa na mauaji makubwa zaidi ya kimbari kuwahi kutekelezwa katika historia ya jeshi la utawala wa Kizayuni, ni hatua muhimu na inayopasa kupongezwa; kwa sababu kupasishwa azimio hilo kunaifanya Palestina itambuliwe rasmi kama cha nchi iliyo na sifa za kuwa mwanachama kamili. Kuhusiana na suala hili, Mohamed Abushahab, Mwakilishi wa Kudumu wa Imarati (UAE) katika Umoja wa Mataifa ambaye aliwasilisha rasimu hiyo akiwakilisha kundi la nchi za Kiarabu ameeleza kuwa wananchi wa Palestina ni watu wanaopenda amani na wanastahili fursa ya kutumikia ubinadamu ipasavyo kupitia Umoja wa Mataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imekaribisha na kuunga mkono juhudi za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupasisha rasimu ya azimio kuhusu uanachama kamili wa Palestina katika taasisi hiyo na kueleza kuwa ufumbuzi wa pande zote wa kadhia ya Palestina unawezekana tu iwapo raia hao watapatiwa haki yao kamili ya kujiainishia mustakbali wao na kuunda nchi huru ya Palestina mji mkuu wake, ukiwa Quds Tukufu. Harakati za kidiplomasia kwa lengo la kuitambua rasmi nchi huru ya Palestina na uanachama wake kamili ndani ya Umoja wa Mataifa ziliongezeka na kushika kasi baada ya kushtadi mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza katika miezi ya karibuni. Pamoja na hayo lakini, Aprili 18 iliyopita wakati nchi 12 wanachama wa Baraza la Usalama zikiwemo Russia na China zilipolipigia kura ya ndio azimio la kukubali Palestina kuwa mwanachama kamili katika Umoja wa Mataifa; Marekani ililipigia kura ya turufu azimio hilo. Hii ni katika hali ambayo nchi 140 kati ya wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa sasa zimeitambua rasmi nchi huru ya Palestina; ambapo Palestina ina balozi na wawakilishi wake wa kudumu katika nchi 95 duniani. Kwa sababu hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuunga mkono uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, inaamini kwamba, kufikiwa jambo hilo ni hatua muhimu katika kukabiliana na dhulma na ukandamizaji wa kihistoria dhidi ya wananchi wa Palestina. Hii ni katika hali ambayo Palestina hivi sasa ni nchi mtazamaji wa kudumu katika Umoja wa Mataifa. Nchi hizo zilizo na hadhi ya waangalizi pamoja na kuwa zinaweza kushiriki katika mikutano mingi, lakini hazina haki ya kupiga kura. Nukta yenye umuhimu kuhusu uungaji mkono wa wazi wa nchi mbalimbali kuhusu kuimarishwa nafasi ya Palestina katika Umoja wa Mataifa ni hii kwamba kumeongezeka uungaji mkono wa nchi nyingi duniani baada ya vita vya Gaza na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni; na hilo linaweza kutajwa kuwa moja ya taathira za mauaji ya kimbari na jinai kubwa za kikatili zinazofanywa na Wazayuni huko Gaza.
Kwa hakika, licha ya nchi za Magharibi kushirikiana na kuihami Tel Aviv kwa upande mmoja, na nchi hizo kufanya kila ziwezalo ili kukwamisha kuimarishwa haki za taifa la Palestina kama nchi mwanachama rasmi wa Umoja wa Mataifa kwa upande wa pili, lakini hali ya mambo imekuwa kinyume na matakwa yao na ya utawala wa Kizayuni. Aidha suala la kupandishwa uanachama wa Palestina katika taasisi muhimu zaidi ya kimataifa limefikiwa kutokana na msisitizo na ufuatiliaji wa jamii ya kimataifa na inatarajiwa kuwa kuendelea kwa mchakato huu katika siku zijazo kutaliwezesha taifa la Palestina kunufaika na haki zake kamili katika chombo hicho muhimu zaidi duniani sawa na nchi nyingine.