Jun 24, 2023 11:18 UTC
  • Al Hashdu Shaabi ya Iraq yawatia mbaroni viongozi 3 wa Daesh

Harakati ya wapiganaji wa kujitolea ya wananchi wa Iraq maarufu kama Al Hashdu al Shaabi (PMU) imetangaza kuwatia mbaroni viongozi watatu wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika mkoa wa Kirkuk nchini humo.

Mwaka 2017 baada ya kupita miaka mitatu na nusu, Iraq ilitangaza ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) ambalo lilikuwa limeikalia kwa mabavu theluthi moja ya ardhi ya nchi hiyo. Hata hivyo licha ya ushindi huo, masalia na mabaki ya magaidi wa kundi hilo yangali yanatekeleza vitendo vya kigaidi katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na katika mikoa ya Kirkuk, Salahuddin, al Anbar na Diara. 

Viongozi 3 wa Daesh wakamatwa Kirkuk 

Harakati ya al Hashdu Shaabi leo imetoa taarifa ikitangaza kuwa wapiganaji wake wake wamewatia nguvuni magaidi watatu wa Daesh katika oparesheni iliyofanyika katika mkoa wa Kirkuk kaskazini mwa Iraq. Magaidi hao wa Daesh walishiriki katika shambulizi la wiki mbili zilizopita kwenye makao makuu ya Jeshi la Iraq. 

Jumapili ya tarehe 11 mwezi huu wa Juni pia duru za Iraq zilitangaza kuwa kundi la Daesh limehusika katika shambulio dhidi ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo karibu na eneo la al Debs mkoani Kikruk ambapo waliwauwa wanajeshi watatu na kujeruhi wanajeshi wengine watatu wa Syria. 

Tags