Kumbukumbu ya Kuzaliwa Bibi Zaynab al Kubra AS
(last modified Sun, 14 Feb 2016 08:11:53 GMT )
Feb 14, 2016 08:11 UTC
  • Kumbukumbu ya Kuzaliwa Bibi Zaynab al Kubra AS

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) binti ya Imam Ali bin Abi Talib (a.s); mwanamke ambaye aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na fadhila, elimu, subira na ushujaa mkubwa aliokuwa nayo. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab (a.s) hapa nchini imepewa jina la "Siku ya Wauguzi".

Bibi Zaynab al-Kubra (a.s) alizaliwa tarehe 5 Mfunguo Nane Jamadul Awwal mwaka wa 5 au wa 6 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Mwaka huu tunaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zaynab mjukuu wa Mtume saw katika hali ambayo haram yake tukufu kwa sasa ina mazingira tofauti katika mji wa Damascus nchini Syria. Katika miaka hivi ya karibuni ya vita na machafuko huko Syria eneo hilo takatifu mara kadhaa limekabiliwa na mashambulio ya makundi ya kitakfiri. Bibi Zaynab (a.s) anayejulikana kama Shujaa wa Karbala na mbeba bendera ya harakati baada ya kuuawa shahidi ndugu yake yaani Imam Hussein bin Ali (a.s), alizaliwa na kulelewa katika nyumba iliyokuwa imejaa huba, fadhila na utukufu yaani nyumba ya Bibi Fatima Zahra na Imam Ali bin Abi Twalib (a.s). Bibi Zaynab (as) alirithi matukufu yote kutoka kwa baba yake yaani Imam Ali (a.s) na mama yake Bibi Fatima (a.s). Akiwa chiniya usimamizi na uangalizi wa malezi ya moja kwa moja ya wazazi wake hao watukufu aliweza kukwea na kufikia daraja za juu za utukufu, ubora na ukamilifu. Bibi Zaynab (a.s) alijifunza upole na uvumilivu kutoka kwa kaka yake Imam Hassan (as) huku akijifunza ushujaa kutoka kwa Imam Hussein (as). Ni kutokana na sifa hizo bora ndipo ikadhihiri nuru na utukufu wa Kiislamu katika haiba ya mwanamke huyo mwema.
Bi Zaynab AS aliondokea kuwa na taqwa, subira, kufungamana na maadili mema na sifa nyingine njema ambazo alijifunza kutoka kwa mama yake mwema ambaye ni mbora wa wanawake yaani Fatima Zahra AS. Bibi Zaynab (as) aliipitisha sehemu ya utoto wake kando ya babu yake yaani Mtume SAW na kupitisha moja ya vipindi vilivyojaa kumbukumbu nzuri. Hata hivyo kipindi hicho hakikudumu, kwani Bwana Mtume SAW aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake. Aidha haukupita muda mrefu, mama yake naye akarejea kwa Mola wake. Licha ya kuwa Bibi Fatima Zahra (as) hakupitisha muda mrefu sana akiwa pamoja na watoto wake; lakini katika kipindi hicho hicho kifupi alichokuwa nao, aliwafunza watoto wake hao somo la juu kabisa la kumuabudu Mwenyezi Mungu na kutetea haki. Darsa yake ilijaa hamasa na ikhlasi na mwalimu huyo alikuwa akifanya hima kubwa ya kuwafundisha wanawake akhlaqi ya Kiislamu kwa mbinu ya kivitendo.
Sayyida Zaynab (as) alikuwa na akili ya hali ya juu, kiasi kwamba, katika kipindi hicho hicho cha utoto na kuinukia kwake aliweza kuhifadhi kwa moyo hotuba aali na iliyojaa madhumuni makubwa ya mama yake katika msikiti wa Mtume SAW yaani Masjdun Nabi. Hiyo ilikuwa ishara ya wazi ya upana wa fikra na hali ya kupevuka kifikra ya binti huyo aliyekulia katika maktaba ya Wahyi. Kielimu, Bibi Zaynab (as) alikuwa amebobea mno kiasi kwamba, umashuhuri wa elimu yake uliwafanya wanaume na wanawake wa Bani Hashim wampe lakabu ya "Mwanamke Mwenye Hekima."
Kwa hakika Zaynab (as) alikuwa mashuhuri miongoni mwa watu kutokana na maarifa na elimu kubwa aliyokuwa nayo. Katika tukio la Karbala, Bi Zaynab (as) alisimama kidete na kukabiliana barabara na dhulma za watawala madhalimu na majahili wa zama hizo ili kutimiza malengo matukufu ya kaka yake, Imam Hussein (as). Wanawake na mabinti wa Madina walikuwa wakienda katika nyumba ya Bibi Zaynab kwa ajili ya kujifunza elimu na maarifa. Zaynab kwa upande wake alikuwa akiitumia fursa hiyo kuwabainisha masuala mbalimbali ya kidini, kijamii na kisiasa. Darsa hizo za elimu ziliendelea pia wakati Bi Zaynab alipokuwa mjini Kufa baada ya baba yake kuelekea katika mji huo. Katika zama hizo wanawake na mabinti waliokuwa na hamu, shauku na raghba ya elimu walimtumia ujumbe Imam Ali AS na kumueleza kwamba, tumesikia kwamba, binti yako Zaynab kama alivyokuwa mtukufu mama yake, ni chemchemi ya elimu na maarifa na ana elimu na ukamilifu; hivyo turuhusu tuje kwake na kunufaina na elimu yake.
Bi Zaynab kama walivyo watu wengine wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW hakuwa nyuma katika masuala ya kiibada, dua na kunong'ona na Mwenyezi Mungu. Alitambulika kuwa mchaji Mungu na mtu aliyezama katika ibada na uchaji Mungu. Alikuwa akiamka nyakati za usiku na kuacha usingizi na kisha kusimama akifanya ibada na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mbali na Swala za usiku alikuwa akisoma mno kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani Tukufu. Baada ya tukio la Karbala licha ya masaibu, machovu, mateso na taabu alizokabiliana nazo yeye pamoja na watu wengine wa familia ya kaka yake yaani Imam Hussein (as), katu hakusahau au kughafilika kusali Swala za usiku. Imam Sajjad (as) anasimulia akisema: Shangazi yangu Zaynab (as) alikuwa akisali Swala zake zote za wajibu na mustahabu tukiwa njiani kutoka Kufa tukipelekwa Sham; na baadhi ya wakati alikuwa akitekeleza taklifu hizo za kidini akiwa amekaa kutokana na njaa kali na kudhoofika mwili."
Sifa nyingine kubwa ya Bi Zaynab AS ni uvumilivu na subira isiyo ya kawaida aliyokuwa nayo. Aidha aliondokea kuwa mashuhuri kutokana na kuwasaidia wahitaji na wasiojiweza na inaelezwa kwamba, nyumba yake mjini Madina ilikuwa kimbilio la wasio na uwezo na waliokwama katika mambo yao.
Mmoja wa watafiti anaandika kuhusiana na hali hiyo kwa kusema: "Muamala na radiamali ya Bibi Zaynab (as) dhidi ya maadui, ilikuwa ya kushangaza na kustaajabisha. Aliweza kuwahutubu kwa maneno makali mno viongozi jeuri, licha ya wao kuwa na madaraka na uwezo mkubwa. Kwa sauti ya juu, aliweza kuitikisa kasri ya kidhalimu na ghasibu ya Bani Umayya, sanjari na kuifedhehesha majlisi ya Yazid kwa maovu yake kupitia hotuba aliyoitoa mbele yake na watu wake wa karibu." Aidha miongoni mwa sifa nyingine adimu za Bibi Zaynab (as) ni ushujaa wa hali ya juu aliokuwa nao. Mtukufu huyo alisimama kwa nguvu zake zote na kupambana na madhalimu na hata kufikia kupewa lakabu ya "Simba wa Bani Hashim." Katika majlisi ya Ibn Ziyad, mtawala wa mjini Kufa Iraq, Bibi Zainab (as) bila kujali kuwa mtawala huyo aliyekuwa na kila uwezo wa kidhahiri, alikuwa amekaa kwenye kasri lake, huku bila kuzingatia maswali aliyoyatoa Ibn Ziyad, Bibi Zainab (as) alimdhalilisha mtawala huyo na kumwita fasiki na mwovu. Akijibu maneno ya kejeli ya Yazid dhidi ya ushujaa wa Bani Hashim, Bibi Zainab alisema: "Nakuona mdogo zaidi ya ninavyoweza kukusifia, lakini nifanyeje kwa zama ambazo watu wamekengeuka njia ya haki na kukutawalisha wewe juu yao, ukapata uwezo wote huu na kuweza kumuua shahidi mjukuu wa Mtume na kuwachukua mateka watu wa familia yake..."
Bibi Zainab (as) alishuhudia tukio chungu, gumu, la kusikitisha na la kihistoria la Karbala. Wakati alipouawa shahidi Imam Hussein na wafuasi wake 72, Bibi Zainab (as) alibeba jukumu zito kabisa la tukio hilo. Mbali na hayo alikuwa na jukumu la kuwaongoza manusura wa Ahlul-Bayt wa Mtume (saw) kutoka mjini Karbala hadi Sham, na kutoka Sham hadi mjini Madina. Licha ya kutokea tukio la siku ya Ashura huko Karbala, lakini Bibi Zainab (as) alikabiliana nalo kwa msingi wa ridhaa ya Mwenyezi Mungu na tokea kujiri kwa tukio hilo hadi kufa kwake, hakulalamikia jambo lolote, bali alisikika akimshukuru tu Mola wake. Kwa mfano, siku chache baada ya kujiri mauaji ya Karbalaa, akiwa katika kasri la kidhalimu mjini Kufa, Ibn Ziyad alimkejeli Bibi Zainab kwa kusema: "Umeona vipi hekima ya Mwenyezi Mungu juu ya Ahlul-Bayt?" Mtukufu huyo akamjibu kwa kusema: "Sikuona kitu kingine ila uzuri."
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnsaba wa kukumbuka siku aliyozaliwa Sayyida Zaynab AS binti wa Imam Ali bin Abi Talib AS, siku ambayo kama tulivyaoshiria mwanzoni mwa kipindi hiki maalum huadhimishwa hapa nchini kama "Siku ya Wauguzi".

Tags