Kupunguzwa wanadiplomasia wa Iran; mchezo wa Kuwait katika uwanja wa Saudia
Baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait kuchukua uamuzi wa kupunguza idadi ya wanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu nchini humo, balozi mdogo wa nchi hiyo mjini Tehran ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kufahamishwa kuwa serikali ya Iran pia ina haki ya kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya Kuwait.
Kuhusiana na kinachotajwa kuwa faili la Abdali, ambalo linasemekana kuwa ni kundi la kigaidi lililo na uhusiano na Iran, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait siku ya Alkhamisi ilichukua hatua ya kupunguza idadi ya wanadiplomasia wa Iran wanaohudumu nchini humo. Bahram Qassimi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema inasikitisha kuona kuwa viongozi wa Kuwait katika mazingira tata ya hivi sasa katika eneo, badala ya kufanya juhudi za kupunguza mivutano na kuwa na subira mbele ya mashinikizo na harakati za kichochezi katika eneo, wamesalimu amri mbele ya harakati hizo na kutoa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran. Kwa mara nyingine tena Qassimi amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina uhusiano wowote na faili la Abdali na kwamba tayari ilikuwa imeshawabainishia wazi jambo hilo viongozi wa Kuwait mwanzoni mwa uchunguzi wa faili hilo.
Faili la kundi la Abdali lilifunguliwa mwaka 2015 katika moja ya mahakama za Kuwait ambapo viongozi wa nchi hiyo wanalituhumu kundi hilo kuwa linahusika na ujasusi na ugaidi, na kisha kulihusisha na Iran.
Swali linaloulizwa hapa ni hili kuwa je, ni kitu gani ambacho kimewasukuma viongozi hao kuhuisha tena faili hilo tena katika mazingira tata ya hivi sasa katika eneo la Mashariki ya Kati linashuhudia harakati hatari na haribifu za maadui? Kuimarishwa uhusiano wa Iran na Kuwait na hasa baada ya uvamizi wa utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq nchini humo ni jambo linalobainisha wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikichukua hatua za uwajibikaji za kuunga mkono Kuwait hata katika mazingira magumu ya vita vya kivamizi. Siasa za kirafiki za Iran kwa Kuwait katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikiathiriwa na harakati haribifu na za kichochezi lakini pamoja na hayo Iran daima imekuwa na mtazamo wa kimantiki kuhusu nchi hiyo. Iran siku zote imekuwa ikifuatilia siasa za kulinda uwiano wa kieneo na kusisitiza juu ya kutatuliwa matatizo yaliyopo kupitia mazungumzo. Ushirikiano na fikra ya pamoja kuhusiana na masuala mbalimbali ya kieneo ni msingi muhimu ambao Iran imekuwa ikiufutilia katika siasa zake za nje na hasa kuhusiana na nchi jirani za Ghuba ya Uajemi.
Limekuwa jambo la kawaida kwamba kila mara migogoro inapozuka katika eneo, Iran kwanza huishauri Kuwait. Kwa mfano katika mgogoro wa hivi sasa yaani wa kukatwa uhusiano wa Qatar na nchi nne za Kiarabu Iran haikupoteza wakati katika kuanzisha mashauriano na Kuwait kwa lengo la kutatua mgogoro huo kwa njia ya amani. Kuzingatia uthabiti na usalama wa kudumu pamoja na ujirani mwema katika eneo ni nguzo mbili muhimu zinazotiliwa maanani na Iran kwa ajili ya kutaua mizozo na changamoto za eneo hili nyeti la Ghuba ya Uajemi, na daima imekuwa ikiwajibika vilivyo katika uwanja huo.
Katika upande wa pili, kuna nchi fulani katika eneo hili ambazo zinafuatilia siasa za kichochezi na vurugu kwa madhumuni ya kuharibu uhusiano wa nchi za eneo ili ziweze kunufaika na kudhamini maslahi yao haramu. Hivi karibuni hatua ya Saudi Arabia kuitaka Qatar ibadili siasa zake za nje ilichukuliwa kwa lengo hilohilo. Mashinikizo yanayotolewa dhidi ya Qatar ili ikate uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ikhwanul Muslimeen na kufunga kituo cha kijeshi cha Uturuki mjini Doha yote hayo yanafanyika kwa ajili ya kufikia lengo hilohilo la kudhamini maslahi binafsi.
Saudia imekuwa ikizitia hofu isiyo na msingi nchi nyingine za Ghuba ya Ujemi ili kuvuruga hatua za uwajibikaji za Iran katika kutatua matatizo ya eneo na ili kufikia lengo hilo imekuwa ikitoa tuhuma nyingi zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua ya Kuwait ya kupunguza idadi ya wanadiploamasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo kwa kisingizio cha faili la Abdali kwa hakika ni kusalimu amri na kuamua kuchezea kwenye uwanja wa Saudia, jambo ambalo hadi sasa Qatar imekataa kulikubal, na kusisitiza kwamba haiko tayari kuweka siasa zake za nje katika udhibiti wa Saudia inayohudumia maslahi ya maadui wa Uislamu.