Uhispania kutazama upya mazingira ya kuiuzia silaha Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i47444-uhispania_kutazama_upya_mazingira_ya_kuiuzia_silaha_saudi_arabia
Sambamba na kuendelea uvamizi na hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambayo imekuwa ikisababisha mauaji ya kikatili dhidi ya raia na hata watoto wadogo, serikali ya Uhispania imetangaza kuwa, inatazama upya mazingira ya kuiuzia silaha na zana za kijeshi Riyadh pamoja na mataifa mengine yaliyoko katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 14, 2018 22:02 UTC
  • Uhispania kutazama upya mazingira ya kuiuzia silaha Saudi Arabia

Sambamba na kuendelea uvamizi na hujuma ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen ambayo imekuwa ikisababisha mauaji ya kikatili dhidi ya raia na hata watoto wadogo, serikali ya Uhispania imetangaza kuwa, inatazama upya mazingira ya kuiuzia silaha na zana za kijeshi Riyadh pamoja na mataifa mengine yaliyoko katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud.

Kupitia taarifa yake maalumu, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Uhispania imezitaka pande zote katika vita vya Yemen ziheshimu misingi na sheria za kijeshi na kibinadamu. Viongozi wa Uhispania wametangaza kwamba, kutokana na agizo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Madrid itatazama upya mazingira ya uuzaji silaha na imezitaka pande zote katika vita vya Yemen ziheshimu na kuchunga misingi inayotawala katika sheria za kijeshi na kibinadamu.

Taarifa hiyo imetolewa katika hali ambayo, baada ya jinai zilizofanywa na Saudi Arabia dhidi ya watoto huko Dhahyan nchini Yemen, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Uhispania isimamishe kuiuzia silaha Saudia.

Image Caption

Jinai za Saudi Arabia zimekuwa zikifanyika kwa uungaji mkono wa Marekani kwa Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia na utiwaji saini mikataba mikubwa ya kijeshi na zana za silaha katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kati ya Riyadh na Marekani pamoja na madola ya Ulaya. Hatua hizo zimeufanya utawala wa Aal Saud uzidi kutanua siasa zake za kivamizi siku baada ya siku katika eneo la Mashariki ya Kati.

Vita vya Yemen ni mfano wa wazi wa siasa za kivamizi za Saudi Arabia. Ripoti ya karibuni kabisa ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, tangu Muungano wa Kiarabu ulipoanzisha vita huko Yemen, zaidi ya raia 17,000 wameuawa huku wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa, mamilioni ya raia wa Yemen wamekuwa wakimbizi. Vilevile kutokana na athari ya vita na hujuma hiyo ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia, nchi ya Yemen kwa sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa huku kukiweko na taarifa za kuibuka maradhi mbalimbali katika nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Muhammad bin Salman alipokuwa Uhispania mwezi uliopita kutiliana saini mkataba wa kijeshi

Marekani, Uhispania, Ubelgiji, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ni wauzaji wakuuu wa silaha kwa Saudi Arabia. Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, nchi zinazounda muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia huko Yemen, mwaka uliopita wa 2017 zilinunua silaha zenye thamani ya Euro milioni 361 kutoka Uhispania peke yake, ambapo hisa ya Saudia ilikuwa Euro milioni 270.

Mwezi uliopita wa Julai pia, Saudi Arabia ilitiliana saini mkataba wa kijeshi na shirika moja la kijeshi la Uhispani uliokuwa na thamani ya Euro bilioni mbili kwa shabaha ya kununua manowari tano za kivita aina ya Avante 2200 kwa ajili ya kikosi cha majini cha Riyadh. Kuendelea uvamizi wa Saudi Arabia na kushtadi vita nchini Yemen, kumepelekea kuibuka wimbi la maandamano na malalamiko ya makundi ya kiraia na wanaharakati wa haki za binadamu katika nchi mbalimbali za Ulaya. Waandamanaji hao wanasema kuwa, akthari ya serikali za Ulaya na Marekani kutokana na kufunga kwao mikataba mikubwa ya silaha na Saudia pamoja na washirika wake zimekuwa zikisaidia kuchochea moto wa vita hususan dhidi ya Yemen na uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi kama Daesh.

Mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya watoto wa Yemen

Robert Fisk, mwandishi wa gazeti la Independent anaandika kuhusiana na suala hilo kwamba: Kumepatikana nyaraka nchini Syria zinazoonyesha kununuliwa silaha na kutumwa silaha hizo kwa makundi ya kigaidi katika nchi hiyo. Malalamiko hayo na kuonyeshwa picha za kuumiza moyo za raia hususan watoto wadogo wasio na hatia waliouawa kinyama katika hujuma ya kijeshi ya muuungano unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen ni jambo lililopelekea kuongezeka mashinikizo dhidi ya serikali zinazoiuzia silaha Riyadh. 

Kwa kuzingatia hilo, baadhi ya nchi za Ulaya ikiwemo Uhispania zimetangaza kuwa, zitatazama upya suala la kuiuzia silaha Saudi Arabia. Bénédicte Jeannerod, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch nchini Ufaransa anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Endapo Ulaya itaendelea kuiuzia silaha Saudi Arabia, itakuwa mshirika wa nchi hiyo ya Kiarabu katika jinai zake za kivita.