Kuchomwa moto Qur'ani Tukufu, balozi wa Sweden atimuliwa Iraq
(last modified Fri, 21 Jul 2023 02:40:23 GMT )
Jul 21, 2023 02:40 UTC
  • Kuchomwa moto Qur'ani Tukufu, balozi wa Sweden atimuliwa Iraq

Serikali ya Iraq imemfukuza balozi wa Sweden mjini Baghdad kulalamikia serikali ya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi ya kuruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Hatua hiyo kali ya serikali ya Iraq ya kumtimua balozi wa Sweden imekuja baada ya jeshi la polisi la nchi hiyo ya Ulaya kumpa idhini tena Salwan Momika kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu na bendera ya Iraq mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' al Sudani amesema katika kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri kilichofanyika jana mjini Baghdad kwamba, kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu si kitu kinachoweza kuvumilika na amemtaka balozi wa Sweden afungashe virago na aondoke Iraq haraka iwezekanavyo.

Waziri Mkuu wa Iraq aidha ameiamrisha Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo kumrejesha nyumbani haraka iwezekanavyo balozi wa Iraq aliyeko Sweden.

Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' al Sudani

 

Hivi karibuni afisa mmoja wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq aliionya serikali ya Sweden kwamba kama itaruhusu tena kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu, basi Iraq itakata uhusiano wake na nchi hiyo ya Ulaya Magharibi.

Mamia ya wananchi wa Iraq walifanya maandamano jana mjini Baghdad wakauvamia ubalozi wa Sweden na kuuchoma moto.

Serikali ya Stockholm imejifanya kukasirishwa na kuchomwa moto ubalozi wake mjini Baghdad, wakati yenyewe huko Sweden inaruhusu na kutoa ulinzi wa kijeshi kwa mtenda jinai anayokivunjia heshima na kukichoma moto Kitabu Kitakatifu cha Waislamu bilioni mbili ulimwenguni.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni baadhi ya nchi za Ulaya hasa za Scandinavia zimeanzisha wimbi la kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu bila ya sababu yoyote zaidi ya chuki zao tu kwa dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu.