Jun 29, 2016 04:26 UTC
  • Ban: Israel inawaumiza Wapalestina kwa mzingiro wake Ghaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amelaani mzingiro wa Israel huko Ukanda wa Ghaza na kusema unawaumiza Wapalestina na kuharibu uchumi wao.

Ban ameikosoa Israel Jumanne wakati alipotembelea Ukanda wa Ghaza na kuhutubia waandishi habari katika shule ya al Zaytoun ambayo inasimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kutoa Misaada kwa Wakimbizi Wapalestina (UNRWA).

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo utaendelea kuwaunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel uliweka mzingira wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Hamas kuongeza eneo hilo. Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani.

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa.

Wakati huo huo kiongozi wa ngazi za juu wa Hamas, Ahmad Bahar amemtaka Ban Ki-moon kuchukua hatua za kivitendo kumaliza mzingiro wa Israel dhidi ya Ghaza. Aidha amekosoa safari ya Ban huko Ghaza na kusema ni katika fremu ya njama za kuzima mwamko na Intifadha ya Wapalestina na kuwashinikiza walegeze misimamo kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Amesema Umoja wa Mataifa umenyamazia kimya jinai za Israel huko Ghaza kwa miaka 10 sasa.

 

Tags