Ansarullah: Kuondolewa serikali madarakani limekuwa takwa la wananchi
(last modified Mon, 02 Oct 2023 08:07:36 GMT )
Oct 02, 2023 08:07 UTC
  • Ansarullah: Kuondolewa serikali madarakani limekuwa takwa la wananchi

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imesisitiza kuwa, kuondolewa madarakani serikali ya Abdul Aziz bin Habtoor limekuwa matakwa la wananchi.

Katika taarifa yake Jumatano iliyopita, Baraza la Ulinzi la Kitaifa la Yemen lilitangaza kuiondoa madarakani serikali ya sasa yenye makao yake makuu mjini Sana'a, inayoongozwa na Abd al-Aziz bin Habtoor na kuikabidhi jukumu pekee la kusimamia kwa muda masuala ya serikali, isipokuwa kuteua na kuwafuta kazi maafisa wa serikali.

Uamuzi wa kuondolewa serikali ya sasa ulichukuliwa na Baraza Kuu la Kisiasa, masaa machache baada ya hotuba ya Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, Ali Al-Khoum, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema, kuondolewa kwa serikali ya Abd al-Aziz bin Habtoor na kuundwa serikali itakayochaguliwa kidemokrasia na wananchi ni jambo la kawaida na takwa la kitaifa, ambalo limetimia kutokana na udharura wa kuundwa serikali ambayo itaboresha utendaji wa taasisi za serikali.

Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah

Al-Kahhoum ameongeza kwamba Abdul Malik Badr al-Din al-Houthi anataka kuundwa serikali kwa ajili ya Wayemeni wote, ambayo itazingatia matakwa ya madhehebu, maeneo na makabila yote na kulinda utambulisho na misingi halisi ya ushirikiano wa kisiasa.

Mjumbe huyo wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameeleza kuwa, masuala muhimu zaidi ambayo yatapewa kipaumbele na serikali ya baadaye ni kutoa huduma, kuleta mabadiliko katika taasisi mbalimbali na vyombo vya  mahakama, kupunguza machungu na matatizo ya wananchi wa Yemen na kuboresha mfumo wa sera za kiuchumi.

Kuhusu mazungumzo na Saudi Arabia, amesema, mazungumzo yanaendelea na bado wana matumaini.