18 Wajeruhiwa katika msongamano mkubwa Makka
Waislamu 18 waliokuwa katika Ibada ya Umrah wamejeruhiwa kufuatia msongamano mkubwa katika mji mtakatifu wa Makka, Saudi Arabia, miezi sita tu baad aya maelfu kupoteza maisha katika Ibada ya Hija mwaka jana.
Tukio hilo lilijiri Ijumaa usiku katika Masjid al Haram mjini Makka ambapo waumini walikuwa wakishiriki katika ibada za Laylat al Qadr katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Gazeti al-Riyadh limeandika kuwa wale waliojeruhiwa wametibiwa papo kwa hapo na kwamba hakuna yeyote aliyelazwa hospitalini.
Tukio hilo limekuja miezi sita tu baada ya Waislamu zaidi ya elfu nne kupoteza maisha katika Ibada ya Hija mwaka jana. Saudia inadai ni watu 770 walipoteza maisha katika tukio hilo la Mina lakini maafisa wa Hija Iran wa wanasema mahujaji 4,700 wakiwemo Wairani zaidi ya 460 walipoteza maisha.
Mashirika ya habari ya kigeni yanasema watu 2,000 walipoteza maisha katika tukio hilo ambalo lilijiri siku chache tu baada ya winchi kuwaangukia mahujaji wengine na kupelekea watu 100 kufariki dunia katika Masjid al Haram.
Iran imekosoa usimamizi mbovu na uzembe wa Saudia katika Hija na imetaka hatua kadhaa zichukuliwe ili kuwalinda mahujaji. Saudia imekataa kutekeleza mapendekezo ya Iran na badala yake imewazuia Mahijaji Wairani kuhiji mwaka huu.