Mfalme wa Jordan ataka kusitishwa vita mara moja Gaza
Mfalme Abdullah II wa Jordan ameitaka jamii ya kimataifa ichukue hatua za dharura za usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza, ili kuzuia kutokea janga kubwa la kibinadamu katika eneo hilo la Wapalestina lililozingirwa.
Mfalme Abdullah wa Jordan alitoa mwito huo jana Jumapili mjini Amman katika mkutano wake na Ursula von der Leyen, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, ambapo walijadili matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.
Mfalme wa Jordan ameeleza bayana kuwa, hatua ya Israel ya kuendelea na vita vyake 'vinavyochukiza' dhidi ya Gaza na kuendelea kukiuka sheria katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu, haitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kushadidisha hali ya mambo katika eneo zima.
Ameyataka madola yenye nguvu kuishurutisha Israel iheshimu sheria za kimataifa, iwalinde raia na iruhusu kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza. Amelaani pia shambulizi la wiki iliyopita la Israel dhidi ya wahudumu wa afya wa Jordan huko Gaza, na kutaja hujuma hiyo kuwa 'jinai ya kutisha.'
Aidha Mfalme Abdullah II wa Jordan kwa mara nyingine tena amesisitizia haja ya kuundwa taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Baytul-Muqaddas. Kadhalika ameutaka utawala ghasibu wa Israel kujiepusha na vitendo ambavyo vinapelekea kuondoka fursa ya kupatikana amani ya kweli huko Palestina.
Licha ya kuuawa shahidi Wapalestina zaidi ya 12,500 tokea Oktoba 7 hadi sasa, lakini baadhi ya madola ya Magharibi huku yakionyesha mshikamano na Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel, Benjamin Netanyahu, yanapinga usitishaji wa vita hivi vya mauaji ya kimbari huko Gaza.
Kwa upande wake, Ursula von der Leyen, Rais wa Kamisheni ya Ulaya amepinga mpango wa kuwahamisha Wapalestina akisisitiza kuwa, hali ya kihistoria na kisheria ya Quds inafaa kulindwa.
Mbali na kugusia juu ya haja ya kutafutwa amani eti kwa misingi ya uundwaji wa mataifa mawili, afisa huyo wa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameipongeza Jordan kwa kuwapa misaada raia wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza.