Israel yaendelea kushambulia hospitali na kambi za wakimbizi Gaza
Kwa akali Wapalestina 100 waliuawa shahidi jana Jumatano na usiku wa kuamkia jana katika mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
Kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar jana ilimnukuu Riyad al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina akisema kuwa: Leo asubuhi (jana Jumatano) watu 52 wa familia ya Qadoura katika eneo la Jabalia wamefagiwa kikamilifu, wameuawa shahidi.
Al-Maliki alisema hayo pambizoni mwa mkutano wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu huko London, mji mkuu wa Uingereza na kuongeza kuwa, shambulio hilo lilijiri katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Palestina amesema, "Nina orodha ya majina yao (mashahidi), wote 52, kuanzia babu hadi wajukuu, wote wamefutwa kikamilifu."
Wakati huohuo, makumi ya Wapalestina wengine waliripotiwa kuuawa shahidi na kujeruhiwa usiku wa kuamkia jana katika shambulizi jingine la utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza, watu wasiopungua sita wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika hujuma hiyo ya juzi usiku mjini Khan Younis. Hata hivyo baadhi ya duru za habari zinasema waliouawa shahidi huko Khan Younis ni zaidi ya watu 50.
Wazayuni wamefanya jinai hizo licha ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza kwa muda wa siku nne ili kutoa fursa ya kufikishwa misaada ya kibinadamu na pande mbili kubadilishana mateka.
Utawala unaokalia Quds Tukufu kwa mabavu uliahidi kutoshambulia au kufanya hujuma dhidi ya mtu yeyote katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza, na kudai kuwa watu watakuwa na uhuru wa kuvuka kutoka kaskazini mwa Gaza kuelekea kusini kupitia barabara ya kitongoji cha Salah al-Din.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Serikali ya Palestina huko Gaza, idadi ya wananchi wa Palestina waliouawa shahidi kwenye mashambulizi ya kikatili ya Israel huko Gaza tokea Oktoba 7 imekaribia 15,000.