Hasara waliyopata Wazayuni katika siku nne zilizopita
Abu Ubeidah, Msemaji wa Brigedi ya al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas alitangaza Jumatatu usiku kwamba wapiganaji wa kundi hilo wameharibu magari 71 ya kijeshi ya Israel na kuwaangamiza wanajeshi wake 16 katika muda wa siku nne zilizopita.
Abu Obeidah amesema kwamba makumi ya askari wengine wa Kizayuni walijeruhiwa katika operesheni hizo, na kuongeza kuwa operesheni nyingine 42 za muqawama, zimepelekea kuangamia makumi ya askari wa jeshi hilo la Wazayuni.
Msemaji wa Brigedi ya Al-Qassam amesisitiza wameweza kutungua ndege mbili zisizo na rubani na kudhibiti nyingine moja.
Abu Ubaidah amesema wapiganaji wa muqawama wameharibu makao makuu na vyumba vya kamandi katika medani na kuvurunga mkusanyiko wa askari hao kwa mizinga na makombora.
Msemaji huyo wa Brigedi ya Al-Qassam ameendelea kusema kuwa Mujahidina pia wameshambulia mji wa Tel Aviv kwa makombora ya M90.
Habari nyingine ni kwamba vyanzo vya utawala wa Kizayuni vilitangaza Jumatatu usiku kwamba maroketi kadhaa yalirushwa kutokea Syria kuelekea Golan inayokaliwa kwa mabavu.
Kufuatia shambulio hilo, ving'ora vya hatari vililia huko Golan na maeneo ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hadi sasa, hakuna habari zaidi zilizotolewa kuhusu shambulio hilo.
Tarehe 7 Oktoba 2023, makundi ya muqawama ya Palestina yalianzisha operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa kutokea Ukanda wa Gaza dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni, na utawala huo kushambulia kwa mabomu maeneo ya makazi, matibabu na kiutamaduni ya Ukanda wa Gaza ili kulipiza kisasi na kufidia kushindwa kwake na vilevile kusimamisha shughuli za makundi ya wanamapambano wa Kipalestina.
Takriban miezi 3 baada ya tukio hilo, utawala haramu wa Kizayuni bado ungali unaendeleza mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya maeneo mbalimbali ya Gaza yakiwemo makazi ya raia na maeneo ya matibabu ili kufidia kipigo hicho cha kihistoria.