Kukamatwa mtandao wa kijasusi wa Mossad nchini Uturuki
Ikiwa ni katika juhudi zinazoendelea za kufuatilia, kufichua na kuvunjwa mitandao ya kijasusi ya Israel nchini Uturuki, serikali ya Ankara kwa mara nyingine imetangaza kuwa mtandao wa kijasusi wa Mossad umegunduliwa nchini humo na baadhi ya wanachama wake kukamatwa.
Kuhusiana na hilo, vyombo vya habari vya Ankara vimeripoti kuwa wanachama 33 wa kundi hilo la majasusi 46 wamefuatiliwa na kukamatwa. Inasemekana kwamba wanachama wa kundi hilo wamekuwa wakitafuta, kugundua na kuwateka nyara watu ambao wanatafutwa na Mossad. Operesheni hiyo ilifanywa na polisi wa Istanbul na vikosi vya usalama katika maeneo 57 katika wilaya 8 za Istanbul, ambapo msako wa kuwakamata wanachama wengine wa kundi hilo la kijasusi ungali unaendelea. Ripoti ya vyombo vya habari vya Uturuki haikutaja utambulisho wa raia hao. Hii si mara ya kwanza kwa shughuli za kijasusi za utawala wa kibaguzi wa Israel kugunduliwa nchini Uturuki. Kabla ya hapo, visa vingi vya shughuli haramu, hususan shughuli za kijasusi za utawala wa Kizayuni nchini Uturuki, vimefichuliwa na kutangazwa hadharani.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, hii ni mara ya tano kwa Shirika la Upelelezi la Uturuki (MET) kukamata mitandao ya kijasusi ya Israel katika nchi hiyo. Ufichuzi huo na kutiwa mbaroni majasusi wa utawala haramu wa Israel kunaonyesha kuwa, utawala huo wa Kizayuni unafanya juhudi kubwa za kijasusi nchini Uturuki kwa madhumuni ya kuendeleza malengo yake hatua kwa hatua na hatimaye kuiangamiza nchi hiyo miongoni mwa nchi za Kiislamu. Awali, kesi nyingi za juhudi zisizo halali, haswa shughuli za kijasusi za utawala wa kibaguzi wa Israel, zilitambuliwa na kutangazwa na vyombo vya habari vya Uturuki. Hii ni katika hali amabayo Uturuki ni miongoni mwa nchi za kwanza kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni baada ya kuasisiwa kwake. Kwa hakika, hakuna nchi yoyote duniani inayochukuiwa na shirika la kijasusi la Israel (Mossad) kuwa rafiki wa utawala wa Israel, bali nchi zote, iwe rafiki au adui, zote kwa pamoja zinachukuliwa kuwa adui wa utawala huo haramu.
Mtandao wa kijasusi wa Israel umekamatwa Uturuki, katika hali ambayo hivi karibuni mitandao mingine miwili ya kijasusi ya Mossad ilitiwa mbaroni nchini humo. Moja ya mitandao hiyo ulikuwa ikifuatilia taarifa na habari zinazohusiana na mashirika ya Kiirani yanayojishughulisha na mambo tofauti nchini Uturuki, na mwingine ukiwafuatilia wanafunzi wa Kipalestina wanaoishi na kusoma katika nchi hiyo. Inaonekana kuwa serikali ya Uturuki haitangazi baadhi ya mitandao ya kijasusi ya Israel inayonaswa nchini. Kwa idadi hii ya kesi za ujasusi, tunaweza kusema kwa yakini kuwa, shughuli za kijasusi za Israel katika miji tofauti ya Uturuki hazipasi kuchukuliwa kuwa suala la kawaida. Ni wazi kuwa si nchi za Kiislamu pekee ndizo zinalengwa na shughuli za kijasusi za Mossad huko Uturuki.
Kwa mujibu wa ufichuzi uliofanywa na viongozi wa zamani wa Uturuki na Marekani, viongozi wa sasa wa Ankara wanapaswa kuzingatia zaidi ukweli kwamba Uturuki ni miongoni mwa walengwa wakuu wa shughuli za mashirika ya kijasusi duniani hususan ya utawala wa Kizayuni. Kwa mtazamo huo, tunaweza kuashiria matamshi ya Madeleine Albright, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani aliyesema wazi kuwa: "Uturuki ni nchi kubwa na haiwezi kubakia kuwa nchi ya Waturuki peke yao". Kwa hakika, mwanasiasa huyo wa kidemokrasia wa Marekani alisema waziwazi miongo miwili iliyopita, kuhusu uwezekano wa kugawanywa Uturuki katika maeneo na nchi kadhaa zinazojitawala. Kwa kuzingatia hayo, hatupaswi kupuuza ukweli kwamba serikali za Magharibi zinazoongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni zinatumia kila mbinu ili kuigawa Uturuki katika sehemu ndogo ndogo zinazojitawala. Pamoja na hayo, inasikitisha kuona kwamba viongozi wa serikali ya Recep Tayyip Erdogan wanaendelea kuimarisha uhusiano na maadui wa uhuru na umoja wa ardhi ya nchi yao.