Kundi la kigadi la Jaishu Dhulm lakiri kushambuliwa ngome zake Pakistan
(last modified Wed, 17 Jan 2024 08:05:56 GMT )
Jan 17, 2024 08:05 UTC
  • Kundi la kigadi la Jaishu Dhulm lakiri kushambuliwa ngome zake Pakistan

Kundi la kigaidi la Jaishu Dhulm limetangaza kuwa ngome zake zimelengwa na kushambuliwa kwa makombora usiku wa kuamkia leo katika mpaka wa Iran na Pakistan.

Shirika la habari la Mehr limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, ndege sita zisizokuwa na rubani (droni) na makombora kadhaa yameshambulia vituo vya genge hilo la kigaidi katika milima ya Baluchestan iliyoko katika mpaka wa Iran na Pakistan. 

Jana usiku, vyombo vya habari vya Iran viliripoti kuwa, ngome mbili muhimu za kundi la kigaidi la Jaishu Dhulm nchini Pakistan zimeshambuliwa na kusambaratishwa kikamilifu. 

Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwa, vituo vya kundi hilo la kigaidi vilivyolengwa vipo katika eneo la Kuhe Sabz, katika mkoa wa Baluchistan nchini Pakistan.

Luteka ya pamoja ya Iran na Pakistan

Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, katikati ya mwezi uliopita, genge hilo la kigaidi la Jaishu Dhulm lilikiri kuhusika na shambulizi la kigaidi kwenye makao ya jeshi la polisi huko Rask, kusini mashariki mwa Iran. Watu 12 waliuawa shahidi katika shambulio hilo la kigaidi lililolenga makao ya jeshi la polisi huko Rask.

Katika hatua nyingine, Vikosi vya Baharini vya Iran na Pakistan vimeendelea kufanya luteka ya pamoja ya kijeshi katika Lango Bahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi. 

Mazoezi hayo ya kijeshi yaliyoanza Jumamosi iliyopita, yanahusisha manowari za kijeshi pamoja na zana nyingine za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan.

Tags