Mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na Netanyahu wazinduliwa rasmi
Duru za Kizayuni zimeshadidia kupamba moto hitilafu kati ya Biden na Netanyahu na zimetangaza kuanza mchakato wa vyama vya utawala wa Kizayuni wa Israel, wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na baraza la mawaziri la Netanyahu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, vyombo vya habari vya Kizayuni vimetangaza kuwa chama cha Yesh Atid kinachoongozwa na Yair Lapid (mkuu wa vuguvugu la upinzani la utawala wa Kizayuni) kimeamua kuwasilisha mpango wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na baraza la mawaziri la Netanyahu kutokana na uvundo lilioufanya kwenye bajeti ya mwaka 2024.
Chama cha Lapid tayari kimesema kuwa serikali ya Netanyahu imefanya uvundo na haifai kupewa nafasi ya kusimamia bajeti ya mwaka huu.
Kabla ya hapo pia, chama cha Labour cha utawala wa Kizayuni kilitangaza kuwa kinakusudia kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na baraza la mawaziri la Netanyahu kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuwakomboa mateka wa Israel huko Gaza.
Hii ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa vita huko Gaza, mipango miwili imewasilishwa kwa wakati mmoja kwa ajili ya kutangaza kutokuwa na Imani na serikali ya Benjamin Netanyahu huko Israel.
Wakati huo huo, maafisa wa Marekani wamesisitiza kwamba mizozo kati ya serikali ya Biden na Netanyahu imeongezeka sana hasa baada ya safari ya hivi majuzi ya Antony Blinken waziri wa mambo ya nje wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
Duru hiyo imesema kuwa, utawala wa Joe Biden huko Marekani unajiandaa na hali ya baada ya kufukuzwa utawala wa Netanyahu ili kufikia malengo yake katika eneo hili.
Duru hiyo imewanukuu maafisa wa Marekani wakisema kuwa, utawala wa Biden, pamoja na baadhi ya maafisa wa Israel, wanajaribu kuandaa hali ya kuundwa baraza jipya la mawaziri baada ya kutimuliwa Netanyahu.