Dunia yaendelea kupinga matamshi ya Netanyahu kuhusu taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107432-dunia_yaendelea_kupinga_matamshi_ya_netanyahu_kuhusu_taifa_la_palestina
Viongozi wa nchi mbalimbali duniani wameendelea kupinga na kukemea matamshi yalitotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akipinga suala la kutambuliwa rasmi taifa huru la Palestina.
(last modified 2024-01-20T07:09:11+00:00 )
Jan 20, 2024 07:09 UTC
  • Dunia yaendelea kupinga matamshi ya Netanyahu kuhusu taifa la Palestina

Viongozi wa nchi mbalimbali duniani wameendelea kupinga na kukemea matamshi yalitotolewa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akipinga suala la kutambuliwa rasmi taifa huru la Palestina.

Katika mkondo huo, Mkuu wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uingereza amelaani kauli hiyo ya Netanyahu akisema kuwa ni hatari.

Ni baada ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutangaza rasmi siku ya Alkhamisi iliyopita kwamba anapinga kuasisiwa taifa huru la Palestina baada ya kumalizika vita vya Gaza. Alidai kuwa ardhi zote zilizo magharibi mwa Mto Jordani zinapaswa kuwa chini ya udhibiti wa usalama serikali ya Israeli.
​Mkuu wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Uingereza, Elisha Kearns, ameliambia gazeti la London Standard kwamba Matamshi ya serikali ya Netanyahu yanazusha mifarakano na ni hatari.

Elisha Kearns ameongeza kuwa: "Hatua ya Netanyahu ya kukataa waziwazi kutambua haki za watu wa Palestina inadhoofisha uungaji mkono wa washirika, inawachokoza majirani na kutuweka mbali na amani."

Wakati huo huo, Brendan O'Hara, msemaji wa uhusiano wa kigeni wa Chama cha Kitaifa cha Scotland, amewataka viongozi wa vyama viwili vikuu vya Uingereza kulitambua rasmi taifa huru la Palestina haraka iwezekanavyo.

Vilevile, kundi la wabunge Mayahudi katika Baraza la Wawakilishi la Marekani limepinga kauli ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye amekataa kuanzishwa taifa la Palestina katika siku zijazo.

Josep Burrell, Mkuu wa Sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, pia amemtuhumu Waziri Mkuu wa Israel kuwa anaharibu juhudi za kutatua mzozo na Palestina.

katika upande mwingine, Stephen Dujarric, Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, jeshi la utawala ghasibu wa Israel linazuia kupelekwa misaada zaidi ya kibinadamu kaskazini mwa Gaza.

Kuhusiana na jinai za kivita za Israel huko Gaza, Dujarric pia amesema: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa daima amekuwa akilaani vikali mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu.

Wizara ya Afya ya Paslestina imetangaza kuwa, Wapalestina zaidi ya 24,700 wameuawa shahidi na wengine 62 elfu na 108 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulizi ya kikatili yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Gaza.