Ansarullah wakabiliana na manowari za Marekani, wapiga moja katika Bahari Nyekundu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i107612-ansarullah_wakabiliana_na_manowari_za_marekani_wapiga_moja_katika_bahari_nyekundu
Wapiganaji wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen wametangaza kuwa wamepiga meli ya kivita ya Marekani na kulazimisha meli nyingine mbili za kibiashara za nchi hiyo kurudi kusini mwa Bahari Nyekundu, katika shambulio la hivi karibuni zaidi la harakati hiyo katika eneo hilo lenye umuhimu wa kimkakati.
(last modified 2024-01-25T04:34:11+00:00 )
Jan 25, 2024 04:34 UTC
  • Ansarullah wakabiliana na manowari za Marekani, wapiga moja katika Bahari Nyekundu

Wapiganaji wa harakati ya Ansarullah nchini Yemen wametangaza kuwa wamepiga meli ya kivita ya Marekani na kulazimisha meli nyingine mbili za kibiashara za nchi hiyo kurudi kusini mwa Bahari Nyekundu, katika shambulio la hivi karibuni zaidi la harakati hiyo katika eneo hilo lenye umuhimu wa kimkakati.

Msemaji wa jeshi la Ansarullah, Yahya Saree, amesema katika taarifa yake iliyosomwa jioni ya jana Jumatano, kwamba wapiganaji wa harakati hiyo wamepambana na manowari na meli za kivita za Marekani katika Ghuba ya Aden na Bab al-Mandab, na kuongeza kuwa mapigano hayo yaliendelea kwa zaidi ya saa mbili, na kwamba walitumia idadi kadhaa ya makombora ya balestiki.

Saree amesema kwamba "meli ya kivita ya Marekani ilipigwa moja kwa moja, na meli nyingine mbili za kibiashara za Marekani zimelazimika kurudi nyuma". Ameongeza kuwa makombora kadhaa ya balestiki yamelenga shabaha kwa usahihi licha ya meli za kivita za Marekani kujaribu kutungua makombora hayo.

Wapiganaji wa Ansarullah wakiteka mojawapo ya meli zinazobeba mizigo ya utawala haramu wa Israel.

Kwa upande wake Mratibu wa Sera za Kistratijia katika Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John Kirby, amedai kuwa Ansarullah walirusha makombora 3 dhidi ya meli katika Bahari Nyekundu, na kwamba mawili yalizuiwa, huku la tatu likikosa shabaha na kuanguka baharini.

Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeanza kushambulia meli za kijeshi za Marekani na Uingereza baada ya nchi hizo mbili kuingilia kati kwa ajili ya kulinda meli za mizigo za utawala haramu wa Israel zinazoshambuliwa na Wayemen kwa lengo la kuulazimisha utawala huo usitishe mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.