Abdollahian aonana na Haniya, asema Wapalestina hawataburuzwa na maajinabi
(last modified Wed, 14 Feb 2024 07:35:38 GMT )
Feb 14, 2024 07:35 UTC
  • Abdollahian aonana na Haniya, asema Wapalestina hawataburuzwa na maajinabi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Wapalestina kamwe hawatakubali kuburuzwa na nchi za kigeni na kusisitiza kuwa, hatima ya taifa la Palestina ipo mikononi mwa Wapalestina wenyewe.

Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo jana Jumanne katika mkutano wake na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Ismail Haniya mjini Doha ambapo wamejadili matukio ya hivi sasa katika Ukanda wa Gaza.

Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa Iran itaendelea na juhudi zake za kidiplomasia za kuunga mkono taifa la Palestina linalodhulumiwa, kwa shabaha ya kukomesha vita, jinai na mzingiro wa Israel dhidi ya Gaza na kukabiliana na njama za kisiasa zinazoupa himaya utawala dhalimu wa Israel.

Haniya kwa upande wake amegusia azma thabiti ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS katika kuendeleza mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Katika kikao chao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kiongozi huyo wa Hamas wamebadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi punde huko Palestina, hususan jinai mpya za Israel mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Abdollahian na Amir wa Qatar mjini Doha

Aidha hapo jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Qatar akiwemo Amir wa nchi hiyo ya Kiarabu, Sheikh Tamim Bin Hamad Al Thani na kusisitizia udharura wa kupunguza mivutano ili kuhakikisha utulivu na usalama unapatikana katika eneo.

Aidha viongozi hao mbali na kupongeza kuzidi kuimarika uhusiano wa pande mbili wa Iran na Qatar, walisisitizia udarura wa kusitishwa mara moja mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza, kuwalinda raia, na kuhakikisha misaada ya kutosha na endelevu ya kibinadamu na ya matibabu inafikishwa kwenye maeneo yote ya ukanda huo.