Qardhawi: Waislamu wajitenge na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11080-qardhawi_waislamu_wajitenge_na_saudia
Mkuu wa unaoitwa Umoja wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani, Sheikh Yusuf Qardhawi ametoa hotuba kali mjini Doha Qatar akimjibu mkuu wa Baraza Kuu la Maulama nchini Saudia, Abdul-Aziz ibn Abdullah Aal ash-Sheikh kwa kujaribu kukilazimisha Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar kifuate siasa za Saudia ikiwa ni pamoja na kupanga njama za kukiua kabisa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2016 23:16 UTC
  • Qardhawi: Waislamu wajitenge na Saudia

Mkuu wa unaoitwa Umoja wa Maulamaa wa Kiislamu Duniani, Sheikh Yusuf Qardhawi ametoa hotuba kali mjini Doha Qatar akimjibu mkuu wa Baraza Kuu la Maulama nchini Saudia, Abdul-Aziz ibn Abdullah Aal ash-Sheikh kwa kujaribu kukilazimisha Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar kifuate siasa za Saudia ikiwa ni pamoja na kupanga njama za kukiua kabisa.

Katika hotuba hiyo Qardhawi pia ameituhumu Saudi Arabia kwa kulikabidhi shirika la G4S la utawala haramu wa Israel jukumu la kusimamia usalama wa Haramu mbili tukufu za Makkah na Madina kupitia makubaliano yaliyofanyika miaka kadhaa iliyopita, ili watawala wa Aal Saudi waweze kuendelea kutawala nchini humo.

Kadhalika mkuu huyo wa unaoitwa Umoja wa Maulama wa Kiislamu Duniani amewataka watawala wa Saudia kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwaua Waislamu katika tukio la Mina kwenye ibada ya Hija ya mwaka huu.

Sheikh Qardhawi ameenda mbali zaidi na kusema kuwa, hii leo suala la kuungana pamoja katika Kamba ya Mwenyezi Mungu, litatimia kwa Waislamu kujitenga na kuwa mbali na utawala wa Aal-Saud na kwamba, mikono michafu ya watawala hao wa Saudi Arabia imetapakaa katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu. Qardhawi ambaye ni sheikh wa Kisalafi na aliyewahi kuwa khatibu mashuhuri wa nchini Misri na hivi sasa nchini Qatar, sanjari na kuwa na misimamo hasi ambapo alifikia hata kuwakufurisha Waislamu wengine, hivi sasa anaonekana kuachana na misimamo yake hiyo ya zamani. Kadhalika msomi huyo amewataka Waislamu kuungana na kuwa kitu kimoja na kuacha mifarakano baina, amewataja watawala wa Saudia kuwa walioimarisha utawala wao kwa kile alichokitaja kuwa ni kwa mifupa ya Waarabu na kupitia mbinu ya kuibua tofauti baina ya Waislamu kama ilivyo leo nchini Yemen, Iraq na Syria.

Amemalizia kwa kusema kuwa, badala ya viongozi hao wa Saudia kuendeleza njia ya shetani wanapaswa kumuomba msamaha Mwenyezi Mungu kutokana na kuwaua wageni wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu na kuacha kuendelea kupanga njama za kuwadhoofisha Waislamu duniani.