Oman: Wahusika wa shambulio la Muscat walikuwa ndugu 3 raia wa Oman
(last modified Fri, 19 Jul 2024 03:50:35 GMT )
Jul 19, 2024 03:50 UTC
  • Oman: Wahusika wa shambulio la Muscat walikuwa ndugu 3 raia wa Oman

Polisi ya Utawala wa Kisultani wa Oman imetangaza kwamba watu watatu waliofanya shambulio kwenye msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Muscat juzi katika siku ya Ashura ya kukumbuuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) walikuwa ndugu wenye utaifa wa Oman.

Taarifa iliyotolewa leo Alkhamisi na Polisi ya Oman imefichua kuwa, watu watatu waliohusika katika ufyatuaji risasi kwenye msikiti mmoja huko Muscat wiki hii walikuwa ndugu raia wa nchi hiyo na kwamba wote watatu wameangamizwa. Taarifa hiyo imesema, uchunguzi umeonyesha kuwa waliathiriwa na fikra potofu.

Polisi wamesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba: "Kwa ajilii ya kujulisha umma kuhusu matukio ya hivi karibuni ya tukio la ufyatuaji risasi huko Wadi Al Kabir, imethibitishwa kuwa watu watatu waliohusika katika tukio hilo ni Waomani na ni ndugu."

"Wameuawa kutokana na kung'angana kupigana na askari usalama, na uchunguzi umeonyesha kwamba waliathiriwa na fikra potofu", imesema taarifa hiyo. 

Japokuwa, taarifa ya Polisi ya Oman haikuweka wazi maana ya "fikra potofu", lakini kundi la kiwahabi na kigaidi la Daesh (ISIS) lilisema katika taarifa yake iliyotolewa kwenye jukwaa la Telegram kwamba ndilo lililohusika na hujuma hiyo.

Shirika la Habari la Oman liliripoti Jumanne iliyopita kwamba hujuma hiyo dhidi ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Muscat iliua watu 9, akiwemo polisi na "wahalifu" 3 na kujeruhi wengine 28.