Mufti wa Oman: Kuiunga mkono Yemen ni wajibu wa kila Muislamu
Mufti Mkuu wa Oman amelaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuushambulia mji wa magharibi mwa Yemen wa al-Hudaydah, huku akiwataka Waislamu kote ulimwenguni kuliunga mkono na kulisaidia kwa hali na mali taifa hilo la Kiarabu linalosumbuliwa na ukata na umaskini mkubwa.
Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili amesema, "Tumeshangazwa na shambulio la adui Mzayuni dhidi ya Yemen; na hujuma hii inafanya kuwa wajibu kwa Waislamu wote kuiunga mkono nchi hii (Yemen) na kuisaidia."
Shirika la habari la Al-Mayadeen limemnukuu Mufti Mkuu wa Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili akisema hayo muda mfupi baada ya ndege za kivita za Israel kushambulia majengo, vituo vya mafuta na kituo cha umeme katika mkoa wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen na kuua watu kadhaa.
Ameeleza bayana kuwa, Yemen imeshambuliwa kutokana na uungaji mkono wake kwa haki za Wapalestina, na kutokana na majibu yake kwa jinai za Wazayuni dhidi ya matukufu ya Kiislamu na taifa la Palestina.
Kadhalika Mufti wa Oman ameashiria jinai za utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kusema, pamoja na ukatili na uhalifu unaofanywa na Wazayun Gaza, lakini tuna matumaini juu ya ushindi mkubwa na wa karibu.

Amesisitiza kuwa, msaada wa chakula tu hautoshi, bali watu wa Gaza wanahitaji pia msaada wa silaha kuweza kukabiliana na mashambulizi na jinai za kila upande za jeshi katili la Israel.
Aidha Mufti wa Oman ametuma salamu za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi raia kadhaa wa Yemen katika shambulio la jana asubuhi la Israel mjini al-Hudaydah huko Yemen, na katika maeneo mengine ya dunia.