Kushadidi mvutano baina ya Uturuki na utawala ghasibu wa Israel
(last modified Wed, 31 Jul 2024 03:04:49 GMT )
Jul 31, 2024 03:04 UTC
  • Kushadidi mvutano baina ya Uturuki na utawala ghasibu wa Israel

Matamshi ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan kuhusu uwezekano wa kuchukua hatua dhidi ya Israel sawa na hatua zilizochukuliwa Karabakh na Libya yameongeza mvutano wa maneno kati ya Ankara na Tel Aviv.

Tangu tarehe 7 Oktoba 2023, utawala wa Kizayuni umeanzisha vita dhidi ya Gaza ambayo hadi sasa imeua na kujeruhi Wapalestina zaidi ya 130,000 wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake. Mashambulizi haya pia yamesababisha kutoweka kwa zaidi ya watu 10,000. Katika hali ambayo, madola ya Magharibi ama yakiwa yamenyamaza kimya mbele ya mauaji ya Kizayuni huko Gaza au yanaunga mkono waziwazi mauaji hayo ya kimbari, baadhi ya nchi za Kiislamu angalau wakati mwingine zinatoa matamshi ya kulaani jinai za Wazayuni na kuunga mkono Gaza.

Akizungumzia jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema siku ya Jumapili kwamba, "Tunaweza kuwafanyia kama tulipokuwa tukiingia Karabakh au kama tulipokuwa tukiingia Libya. Hakuna jambo ambalo hatuwezi kufanya. Tunapaswa kuwa na nguvu tu." Matamshi hayo ya Erdogan yamesababisha kuongezeka kwa mvutano wa maneno kati ya Uturuki na  utawala ghasibu wa Israel.

 

Kufukuzwa kwa balozi wa utawala katili wa Israel na "kuchanganyikiwa" katika sera ya kigeni za  Uturuki 

Vyombo vya habari vya Israel vimeyachukulia matamshi hayo kama tishio la kijeshi. Yisrael Katz,  Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Israel amejibu matamshi ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan. Katz aliweka picha ya Erdogan karibu na Saddam, dikteta wa Iraq, na kuandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba:, "Erdogan anafuata nyayo za Saddam na anatutishia kwa mashambulizi ya kijeshi."

Ameongeza kwa kusema kuwa, kumbuka kilichotokea huko na jinsi kilivyoisha.

Yair Lapid, kiongozi wa upinzani wa utawala wa Kizayuni pia ameeleza kuwa, rais wa Uturuki angali anatoa visingizio na kuzusha utata na ni hatari kwa eneo la Mashariki ya Kati. Lapid ameongeza kuwa: Ulimwengu hasa wanachama wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) wanapaswa kulaani vikali vitisho vya Erdogan dhidi ya Israel na kumlazimisha kukomesha uungaji mkono wake kwa Hamas.

Katika kujibu matamshi hayo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya  Uturuki ilimlinganisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Adolf Hitler na kutangaza: " Kama ulivyokuwa mwisho wa mfanya mauaji ya kimbari Hitler, ndivyo pia utakavyokuwa mwisho wa mfanya mauaji ya kimbari Netanyahu." Katika muendelezo wa taarifa hiyo imesisitizwa kuwa, kama ambavyo Wanazi waliofanya mauaji ya halaiki waliwajibishwa (kwenye meza ya mashtaka), wale wanaojaribu kuwaangamiza Wapalestina nao pia watawajibishwa. Ubinadamu utasimama pamoja na  Palestina na nyinyi hamuwezi kuwaangamiza.

 

 

Rais Erdogan wa Uturuki: Netanyahu mfanya mauaji ya kimbari atakuwa na mwisho kama wa Hitler

Uhusiano kati ya Uturuki na Israel umekuwa na mvutano tena baada ya kuanza kwa vita vya Gaza. Ankara na Tel Aviv zimewaita mabalozi wao na kusitisha biashara na safari za ndege. Wakati huo huo, mabadilishano ya biashara yenye thamani ya dola bilioni 8 yamesimamishwa. Baada ya matamshi haya  mapya ya Erdogan kuchapishwa, baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wa Uturuki wametaka Ismail Haniyeh, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, alikwe mjini Ankara haraka iwezekanavyo ili kutoa hotuba katika bunge la Uturuki na hivyo kwa namna moja kutoa jibu kwa Marekani.

Kwa ombi la Erdoğan, Bunge la Uturuki pia lilishutumu hotuba ya Benjamin Netanyahu katika Bunge la Marekani na kutoa taarifa iliyoeleza kwamba, siasa hizo za Marekani ni kumuunga mkono mtenda jinai muuaji. Waziri wa Sheria wa Uturuki Yilmaz Tunç aliielezea hatua ya Bunge la Uturuki ya kulaani mwaliko wa Netanyahu kwenye Bunge la Congress la Marekani kuwa ni ya kihistoria na kwa maneno ya kutia chumvi, alitangaza kuwa, taarifa hii Bunge la Uturuki imetoa funzo kwa dunia nzima kuhusu demokrasia na haki za binadamu.