Mustafa Ali: UN inabeba dhima ya masaibu yanayowapata watoto Yemen
Mkuu wa Jumuiya ya Watoto nchini Yemen amesema kuwa, Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la umoja huo na asasi za kimataifa zinabeba dhima ya hali mbaya ya kibinadamu nchini Yemen hususan masaibu yanayowapata watoto wa nchi hiyo.
Mustafa Ali amesisitiza kuwa, hali ya kibinadamu nchini Yemen kwa sasa ni mbaya mno kutokana na kuendelea uvamizi na mzingiro wa Saudi Arabia na waitifaki wake.
Mkuu wa Jumuiya ya Watoto nchini Yemen amelaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea kushuhudiwa nchini Yemen hususan dhidi ya watoto na kutahadharisha juu ya kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.
Ameongeza kuwa, kuendelea mzingiro huo na kulengwa miundo mbinu, shule, taasisi muhimu na kusimamishwa harakati za kawaida za maisha nchini Yemen kumepelekea watoto wa nchi hiyo kukosa fursa ya kuishi maisha ya kawaida.
Mkuu wa Jumuiya ya Watoto nchini Yemen ameutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la umoja huo zitekeleze majukumu yao ipasavyo. Mashambulio ya Saudia ikishirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo yalianza mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansur Hadi, Rais wa zamani wa Yemen aliyetangaza kujiuzulu na kukimbia nchi. Hadi sasa maelfu ya wananchi wa Yemen, wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameshauawa huku asilimia kubwa ya miundombinu ikiharibiwa.