Filamu ya 'Madhambi ya Mfalme Fahd' yatengenezwa
Filamu kuhusu ufisadi wa kimaadili na ufuska wa ukoo wa kifalme wa Saudi Arabia, hasa mfalme wa zamani Fahd, imetengenezwa kwa mujibu wa kisa cha kweli.
Trailer ya dakika tatu ya filamu hiyo ya Kiingereza iliyopewa jina la 'The Sins of King Fahd' yaani Madhambi ya Mfalme Fahd' iliwekwa katika mtandao wa YouTube siku ya Ijumaa. Filamu hiyo ambayo inahusu maisha ya mfalme wa zamani wa Saudia aliyefariki, Fahd bin Abdulaziz al-Saud inamuonyesha akijihusisha na vitendo vichafu kama vile kutumia mihadarati, kucheza Kamari n.k.
Filamu hiyo imetengenezwa kwa mujibu wa kisa cha kweli cha Janan Harb ambaye anasimulia maisha yake kama msichana mdogo Mkristo kutoka Palestina aliyekimbia kutoka nchi yake na kujipata Saudi Arabia ambapo alikutana, kutongozwa na hatimaye kuolewa na Mfalme Fahd.
Mwaka jana mahakama moja ya Uingereza iliamuru Saudi Arabia imlipe Harb dola milioni 26.4 kutokana na hatua ya Fahd ya kumpa talaka na kumtimua Saudia pasina kumpa haki zake.
Bi. Harb anasema mfalme wa sasa wa Saudia, Salman bin Abdulaziz, wakati akiwa gavana wa Riyadh ndiye aliyeshinikza apewe talaka na Fahd na kisha kutimuliwa Saudia. Anamtaja Mfalme Salman kuwa, 'Katili wa Riyadh' kwani katika zama zake za ugavana aliwanyonga watu wengi mjini humo.
Harb anasema, mwaka 1968 akiwa na umri wa miaka 20 aliolewa na Fahd ambaye wakati huo alikuwa mritihi wa kiti cha ufalme na waziri wa mambo ya ndani wa Saudia. Amesema, wazazi wake Wapalestina walikuwa wakiishi Riyadh wakati huo na aliweza kumvutia kirahisi Fahd kutokana na kuvaa kwake nguo fupi zilizoonesha maungo ya mwili wake.
Waislamu wengi duniani wamelaani ufisadi huo wa Mfalme Fahd hasa kwa kuzingatia kuwa wafalme wa Saudia kwa kawaida hujipachika anwani ya 'Khadimul Haramein' yaani mhudumu wa Misikiti Miwili Mitakatifu ya Makka na Madina.