Israel yatishia kumuua kigaidi Khalid Mashaal
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel ametoa vitisho kwamba utawala huo wa Kizayuni utamuua kigaidi Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Ughaibuni ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS), Khaled Mash'al.
Kwa mujibu wa gazeti la Misri la al-Sharouq, vitisho vya kumuua kigaidi Khaled Mash'al vimetokana na kuanzishwa tena operesheni za kujitoa muhanga katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Gazeti hilo la Kiarabu limeeleza kuwa, kurejea kwa operesheni hizo za wanamuqawama kumeutia kiwewe utawala huo ghasibu, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yisrael Katz amemtishia maisha Mash'al.
Al-Sharouq imemnukuu Katz akisema kuwa, mamlaka za Israel zitahakikisha kuwa zinatekeleza kwa utimilifu mpango wa kuuawa Khalid Mash'al na wenzake katika uongozi wa HAMAS haraka iwezekanavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel amebainisha kuwa, "Operesheni itakuwa tofauti wakati huu na itafanywa bila mabadiliko hata kidogo."
Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa Julai mwaka huu, utawala katili wa Israel ulimuua kigaidi Ismail Haniyah, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya HAMAS ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na mlinzi wake, shambulio la kigaidi lililolaaniwa kote duniani.