Sep 09, 2024 09:14 UTC
  • Abu Ubaida
    Abu Ubaida

Msemaji wa tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Abu Ubaida, amebariki operesheni ya kishujaa iliyotekelezwa na mwanamapambano raia wa Jordan Shahidi Maher al-Jazi, katika kivuko cha Karama (Allenby) na kumtaja kuwa ni miongoni mwa mashujaa walioshiriki katika Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa Septemba mwaka jana dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abu Ubaida amesema katika taarifa iliyotangazwa kwenye jukwaa la Telegram kwamba, "bastola ya shujaa wa Jordan ya kutetea al Aqsa na watu wetu ilikuwa na ufanisi zaidi kuliko majeshi katili na maghala ya silaha za kijeshi."

Amesisitiza kuwa operesheni hiyo "inadhihirisha dhamiri ya Umma, matokeo ya operesheni Kimbunga cha Al-Aqswa na jinamizi linalowangojea Wazayuni." 

Abu Ubaida amesema kwamba, wapiganaji wa Al-Qassam, tawi la kijeshi la Hamas, wametekeleza Swala ya maiti wakiwa kwenye ngome zao katika Ukanda wa Gaza, kwa ajili ya shahidi na shujaa wa operesheni hiyo."

Wazayuni watatu wa Israel waliuawa jana Jumapili kwa kupigwa risasi karibu na Kivuko cha Allenby (Daraja la King Hussein, kama linavyoitwa Jordan, au Kivuko cha Karama, kama kinavyoitwa upande wa Palestina), kati ya Jordan na Ukingo wa Magharibi, katika operesheni hiyo ambayo ni ya kwanza ya aina yake tangu kuanza mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza Oktoba 7 mwaka jana.