Israel yaunda kikosi maalumu cha kumuua kigaidi Yahya Sinwar
Shirika la kijasusi la ndani la Israel Shin Bet (Shabak) limeunda kitengo maalumu cha kumuua kigaidi Yahya Sinwar, Mkuu mpya wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS.
Kwa mujibu wa ripoti ya IRNA ya Jumapili asubuhi iliyonukuu baadhi ya vyombo vya habari, Kanali ya 12 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni imefichua njama mbaya dhidi ya HAMAS iliyopangwa na Shin Bet.
Kwa mujibu wa ripoti hii, shirika la kijasusi la Israel limeunda na kikosi cha kufuatilia mienendo ya Sinwar, na timu hiyo inafanya kazi saa 24 kumlenga tangu kuanzishwa kwa vita vya Gaza.
Ripoti hii pia imefichua kwamba, chombo cha kijasusi cha utawala wa Kizayuni kimetenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kumsaka Sinwar, ambaye Tel Aviv inaamini kuwa ndiye muasisi wa operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.
Wazayuni wanapanga njama hizi katika hali ambayo, Yahya Sinwar hivi karibuni alisema kuwa, kifo cha mtangulizi wake, Ismail Haniya kimethibitisha kwamba damu ya viongozi wa Muqawama na wapiganaji wake si yenye thamani zaidi kuliko damu ya Wapalestina wengine.
Aidha ameahidi kushikamana na njia iliyofuatwa na Shahidi Ismail Haniya, muhimu zaidi likiwa ni la kuwaunganisha Wapalestina na kuwafanya wawe kitu kimoja katika kushikamana na chaguo la Jihadi na Muqawama na kuepusha migawanyiko na mifarakano.