Wanajeshi wa Kizayuni waangamizwa kusini mwa Lebanon
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon jana ilikabiliana vikali na wanajeshi wa kizayuni na kuishambulia kambi muhimu ya Israel huko kusini mwa nchi hiyo.
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon jana Jumapili ulitoa taarifa ukitangaza kuwa wanamapambano wa Hizbulllah walikabiliana na wanajeshi wa Kizayuni waliokuwa wakijaribu kupenya katika mji wa Belida, kusini mwa Lebanon, na kuua idadi kadhaa ya Wazayuni.

Wakati huo huo, duru za Kizayuni zimeripoti kuwa wanajeshi 22 wa jeshi la utawala huo wamejeruhiwa katika mapigano na wanamuqawama wa Lebanon kusini mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la Kizayuni la Walla limekiri kuhusu kujeruhiwa wanajeshi 25 wa Kizayuni katika mapigano na wapiganaji wa Hizbullah.
Katika taarifa nyingine, Hizbullah imetangaza kuwa: Wanamuqawama wamevurumisha makombora kwenye kituo cha "Tirkamel" kusini mwa Haifa. Hizbullah imesisitiza kuwa iko tayari kuilinda Lebanon na wananchi wa nchi hiyo na haitashindwa kutekeleza wajibu wake wa kukabiliana na adui mchokozi na katili, Israel.