Lebanon yawasilisha malalamiko mapya dhidi ya Israel kwa Baraza la Usalama
(last modified Thu, 17 Oct 2024 02:53:29 GMT )
Oct 17, 2024 02:53 UTC
  • Lebanon yawasilisha malalamiko mapya dhidi ya Israel kwa Baraza la Usalama

Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imesema kuwa imewasilisha malalamiko yake mapya kwa Baraza la Usalama la UN kuhusu utawala wa Kizayuni.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon jana Jumatano ilitangaza katika taarifa yake na kulaani hatua ya utawala wa Israel ya kukiuka mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo na kulishambulia jeshi, wafanyakazi wa huduma za uokoaji na watu wa nchi hiyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon imesema, Utawala wa Israel unafanya kila uwezalo kupitia mabavu na zana zake za kijeshi kuzitwisha nchi za eneo misimamo yake kuhusu usalama wa kanda hii.  

Wizara ya Mambo ya Nje ya Lebanon siku kadhaa zilizopita iliwasilisha kwa Baraza la Usalama la UN malalamiko yake mawili dhidi ya utawala wa Kizayuni. 

Katika malalamiko hayo mawili, Lebanon imetaka kutolewa tamko na kuchukuliwa msimamo mkali mkabala wa shambulio lililofanywa na utawala huo dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Lebanon (UNFIL) na pia kusimamishwa haraka iwezekanavyo mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon ambayo yamesababisha wanafunzi milioni moja na laki nne kushindwa kuhudhuria masomo. 

Jeshi la utawala wa Kizayuni Septemba 23 mwaka huu lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon hujuma ambazo zinaendelea hadi hivi sasa. 

Mashambulizi ya Israel huko Lebanon 

Takwimu za Wizara ya Afya ya Lebanon zinaonyesha kuwa hadi sasa watu zaidi ya elfu mbili na mia tatu wameuliwa shahidi na zaidi ya elfu kumi kujeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni uanzishe mashambulizi dhidi ya nchi hiyo mwezi Oktoba uliopita.

Katika kukabiliana na jinai hizo, Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon pia imefanya mashambulizi mengi katika maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Mashambulizi haya yameibua hofu na taharuki miongoni mwa Wazayuni.