Marekani na Uingereza zashambulia tena Yemen kuunga mkono Israel
Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi mapya ya anga katika mji wa Hudaydah, magharibi mwa Yemen kwa lengo la kuunga mkono utawala haramu wa Israel.
Kanali ya televisheni ya al-Masirah ya Yemen imeripoti leo Alhamisi kwamba mashambulizi hayo ya anga yalilenga eneo lililo karibu na Chuo Kikuu cha Hudaydah katika wilaya ya al-Hawak ya mji huo.
Ripoti hiyo haikutoa habari yoyote kuhusu majeruhi au uharibifu baada ya hujuma hiyo.
Muungano wa kijeshi wa Marekani na Uingereza haujazungumza lolote kuhusu shambulio hilo lililotokea wiki moja baada ya uvamizi sawa na huo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hudaydah.
Marekani na washirika wake wamekuwa wakiishambulia kwa mabomu Yemen katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kinyume cha sheria za kimataifa.
Mashambulizi hayo haramu ya anga yamekuwa yakitekelezwa kujibu operesheni za baharini za majeshi ya Yemen ambazo hutekelezwa kuzuia meli za kibiashra zinazofungamana na utawala haramu wa Israel katika hatua ya mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ambao wanakabiliwa na mauaji ya kimbari ya Israel.
Siku ya Jumanne, vikosi vya wanajeshi vya Yemen vilitekeleza mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani dhidi ya shabaha muhimu katika mji wa Ashkelon katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel.
Katika taarifa, jeshi hilo lilisema kwamba operesheni hiyo ilitekelezwa ili kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa wa Palestina na Lebanon, na harakati zao za muqawama."
Katika kampeni ya kuunga mkono Palestina, vikosi vya Yemen vimelenga idadi kubwa ya meli zinazoelekea au kuondoka katika bandari zilizo katika ardi zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel. Meli hizo zinazousaidia utawala huo kuendeleza mauaji ya Wapalestina zimekuwa zikilengwa kusini mwa Bahari Nyekundu, Mlango-Bahari wa Bab el-Mandeb, Ghuba ya Aden na hata katika Bahari ya Arabia. Pia vikosi vya Yemen vimekuwa vikishambulia meli za Marekani na Uingereza katika maji hayo hayo.
Utawala haramu wa Israeli ulianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023, na kufuatiwa na uchokozi dhidi ya Lebanon.
Hadi sasa utawala huo katili umeshaua Wapalestina wasiopungua 43,163 huko Gaza na Walebanon 2,820 nchini humo. Aghalabu ya waliouawa ni wanawake na watoto.