Matokeo ya kufutwa kazi Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni
Hatua ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ya kumfuta kazi Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala huo imezidisha hali ya mgogoro huko Tel Aviv.
Netanyahu amemfukuza Yoav Gallant na kumteua mahala pake Israel Katz. Netanyahu amekiri kwamba hapakuwa na uaminifu tena kati yake na Gallant, kwa hiyo amemchagua Israel Katz, waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni kuwa waziri mpya wa vita. Gideon Sa'er pia amechaguliwa kuwa waziri mpya wa mambo ya nje wa utawala huo.
Kanali ya Kizayuni ya Kan imeripoti kuwa, Mkuu wa Shabak, Mkuu wa Majeshi na Waziri wa Vita aliyefutwa kazi (Yoav Gallant) wanakabiliana kisiasa moja kwa moja na Benjamin Netanyahu.
Mazungumzo ya Netanyahu na Gallant kuhusu kufukuzwa kwake yalichukua dakika tatu tu, ambapo Netanyahu mwenyewe alimkabidhi mkononi barua ya kufutwa kwake kazi. Tovuti ya Kizayuni ya "Walla" imewanukuu jamaa wa Netanyahu wakisema kuwa anakusudia kuwafuta kazi pia Herzi Halevi, Mkuu wa Majeshi na Ronen Bar, Mkuu wa Shirika la Ujasusi na Usalama wa Ndani wa Israel, Shabak.
Yoav Gallant, katika radiamali yake ya kwanza baada ya kufukuzwa kwake, amesema hivi kama tunavyomnukuu: "Sheria ya msamaha kwa Mayahudi wa Orthodox (Haredis) haikubaliki na ni lazima wapelekwe vitani. Ni lazima tuwakomboe haraka mateka wa Israel (Wazayuni) waliochukuliwa na Hamas. Lengo hili linaweza kufikiwa kwa kutolewa baadhi ya fursa chungu. Kufanya uchunguzi rasmi na wa kimfumo wa kile kilichotokea (tarehe 7 Oktoba 2023) ni jambo la dharura."
Kuondolewa kwa Gallant kumekabiliwa na upinzani mkali wa Wazayuni wenye misimamo ya kupindukia mpaka ambao wamekuwa na hitilafu kali naye katika baraza la mawaziri. Hata hivyo, Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni mwenye misimamo ya kufurutu ada na chuki za kupindukia dhidi ya Waislamu, amekaribisha mabadiliko hayo na kusema: "Natoa pongezi kwa kufukuzwa Yoav Gallant. Hatuwezi kushinda vita tukiwa na Yoav Gallant."
Katika upande wa pili, baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Kizayuni wanaokosoa vikali utendakazi wa Netanyahu katika vita vya Gaza, wamekosoa kufukuzwa waziri huyo wa vita na kuonya kuhusu mgogoro wa kisiasa huko Tel Aviv. Avigdor Lieberman, waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni amesema kuhusiana na kufutwa kazi kwa Gallant kuwa: "Kama imewezekana Waziri wa Ulinzi (Vita) kufutwa kazi katikati ya vita, basi inawezekana pia mtu mwingine kuchukua nafasi ya Waziri Mkuu ambaye ameshindwa kutekeleza majukumu yake."
Naftali Bennett, Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni amejibu hatua ya Yoav Gallant kutimuliwa katika Wizara ya Vita kupitia ujumbe alitoa na kusisitiza: "Benjamin Netanyahu ni mwendawazimu." Yair Golan, Kiongozi wa Chama cha Democrats cha utawala wa Kizayuni pia ametuma ujumbe kwenye mtandao wa X kuhusiana na kuondolewa Gallant katika Wizara ya Vita na kutoa wito wa kufanyika maandamano katika maeneo yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Kuendelea vita vya Gaza kumezidisha mpasuko wa kisiasa huko Tel Aviv, na kuondolewa kwa Gallant katika wizara ya vita bila shaka kutakuwa mwanzo wa kuvunjika baraza la mawaziri la Netanyahu. Pande mbili kuu za baraza la mawaziri, Wazayuni wenye misimamo ya kupindukia mpaka na wale wanaomuunga mkono Netanyahu katika chama cha mrengo wa kulia cha Likud, zimekuwa zikizozana vikali kuhusu kuendelea vita vya Gaza, kwa miezi kadhaa sasa.
Mgogoro wa kiuchumi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Kizayuni umekuwa ukiongezeka kila siku, suala ambalo limechochea malalamiko na maandamano makubwa katika maeneo hayo.
Hatua ya Netanyahu kuvuga mazungumzo ya kusitisha vita huko Gaza pia kumefanya mchakato wa mazungumzo hayo kutatizika na hivyo kusimamisha juhudi za kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni.
Hali ya mgogoro huko Tel Aviv ni matokeo ya uchochezi na uchokozi wa vita wa Wazayuni katika vita vya Gaza. Ndoto ya Netanyahu ya kushinda na kuwatimua Hamas kutoka Gaza imekuwa na madhara makubwa kwa waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni. Aghalabu ya viongozi wa utawala huo pia wamekasirishwa sana na vitendo vyake na kuichukulia hali mbaya ya hivi sasa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kuwa ni matokeo ya kushindwa jeshi la Kizayuni dhidi ya makundi ya muqawama ya Palestina katika vita vya Ukanda wa Gaza.