Rais Aoun: Israel lazima iache kukalia kwa mabavu kusini mwa Lebanon
Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ameitaka Marekani kuushinikiza utawala wa Israel kuacha kukalia kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon.
Aoun alimwambia mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani, Mike Waltz, siku ya Jumatano kuwa ni muhimu kusitisha uvamizi wa Israeli katika ardhi ya Lebanon, kama ilivyokubaliwa chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoihusisha harakati ya Hizbullah.
Rais Aoun amesisitiza kuwa Beirut itachukulia uwepo wowote wa Israel katika ardhi ya Lebanon kama uvamizi.
Makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyopatanishwa na Marekani na Ufaransa, yalieleza kuwa vikosi vya Israeli vinapaswa kuondoka Lebanon kabla ya Januari 26. Hata hivyo, tarehe hiyo iliahirishwa hadi Februari 18 baada ya Israel kukataa kutekeleza makubaliano hayo.
Jeshi la Lebanon, ambalo kwa mujibu wa makubaliano linapaswa kupelekwa katika maeneo ya kusini mwa nchi wakati vikosi vya Israeli vikiondoka, lilisema Jumanne asubuhi kuwa vikosi vya utawala wa Israel bado vinashikilia vijiji kadhaa na maeneo ya mpakani, hata baada ya muda wa kuondoka kumalizika.
Israel imesema itaendelea kuweka vikosi vyake katika "sehemu tano za kimkakati" juu ya vilima vinavyotazama maeneo ya pande zote mbili za mpaka ili "kuhakikisha hakuna tishio la haraka".
Beirut imesema italiomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushinikiza Israel kuondoka, ikisisitiza kuwa Lebanon ina "haki ya kutumia njia zote" kuhakikisha utawala wa Israeli unaondoa kabisa vikosi vyake.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa kutokamilika kwa kuondoka kwa Israel ni ukiukaji wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701.