IOM: Asilimia 90 ya nyumba za Gaza zimebomolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123078-iom_asilimia_90_ya_nyumba_za_gaza_zimebomolewa
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limetangaza kuwa, asilimia 90 ya nyumba katika Ukanda wa Gaza zimeharibiwa, na mamia ya maelfu ya Wapalestina hawana pa kwenda, na Wapalestina ambao wamerejea katika maeneo yao wanajikuta wakikabiliwa na vilima vya uchafu.
(last modified 2025-02-22T23:13:04+00:00 )
Feb 22, 2025 23:13 UTC
  • IOM: Asilimia 90 ya nyumba za Gaza zimebomolewa

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limetangaza kuwa, asilimia 90 ya nyumba katika Ukanda wa Gaza zimeharibiwa, na mamia ya maelfu ya Wapalestina hawana pa kwenda, na Wapalestina ambao wamerejea katika maeneo yao wanajikuta wakikabiliwa na vilima vya uchafu.

Taarifa ya shirika hilo imesema, watu wa Gaza wanaishi katika hali mbaya sana na upatikanaji wa mahitaji na huduma za kimsingi ni karibu sifuri.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema katika taarifa yake kwamba, linafanya kazi na Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu kuongeza misaada ya dharura kwa raia wa Gaza.

Hayo yanaripotiwa baada ya Shirika la Oxfam la Uingereza kutangaza kuwa utawala wa Israel umeharibu zaidi ya asilimia 80 ya mitandao ya maji na maji taka ya Gaza na kusababisha hali mbaya ya kiafya.

Taarifa iliyotolewa na  Clemence Laguarda, mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Oxfam huko Gaza, imesema: "Sasa, baada milipuko ya mabomu kukoma, ndio kwanza tunaanza kuelewa kina cha uharibifu huo mkubwa."

Shirika la Oxfam limeeleza matumaini kuwa usitishaji mapigano utaendelea na kwamba mafuta na misaada ya kibinadamu itafika Gaza ili Wapalestina waweze kujenga upya maisha yao.

Tathmini ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, na Benki ya Dunia inaonyesha kuwa ujenzi mpya wa eneo la Gaza na Ukingo wa Magharibi unahitaji dola bilioni 53.2 katika kipindi cha miaka 10 ijayo.