Hamas yalaani mashambulizi huku Israel ikishambulia Ukingo wa Magharibi
Harakati ya muqawama ya Hamas imelaani uamuzi wa Israel wa kupanua mashambulizi yake ya kijeshi katika Ukingo wa Magharibi wa kaskazini, ikisema kuwa uchokozi huu unaonesha nia hatari ya utawala wa kikoloni wa Israel kuendelea na vita vyake vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.
Jeshi la Israel limeingiza vifaru katika Ukingo wa Magharibi wa kaskazini Jumapili, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2002, huku hali ya kijeshi ikizidi kuzorota katika ardhi hii ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Hamas ilisema, "Uamuzi wa utawala wa Kizayuni kuongeza vitendo vyake vya uchokozi katika Ukingo wa Magharibi, pamoja na kampeni za kuwafurusha kwa nguvu zaidi ya Wapalestina 40,000 katika kambi za wakimbizi za Jenin, Tulkarm, Nur Shams na al-Far’a, unahitaji jamii yote ya Kipalestina na vikundi vyake vya mapambano kuungana dhidi ya uhalifu huu wa kinyama."
Hamas iliongeza kuwa "Kauli za waziri wa vita wa Israel, Israel Katz, kuhusu kuweka vikosi vya utawala huo katika kambi za kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi kwa mwaka mzima na kuwazuia wakazi wake kurudi makwao, ni ndoto ambazo hazitatimia kamwe."
Hamas pia ilitoa wito kwa watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi kuongeza mapambano yao ili kukomesha uhalifu wa Israel.
Tangu mwezi uliopita, jeshi la Israel limekuwa likiendesha operesheni za kijeshi katika Ukingo wa Magharibi wa kaskazini, hali ambayo imesababisha vifo vya angalau Wapalestina 60 na kuwafurusha maelfu ya wakazi.
Mashambulizi haya ni sehemu ya ongezeko la uvamizi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi, ambako takriban Wapalestina 923 wameuawa na karibu 7,000 wamejeruhiwa kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel na walowezi haramu tangu vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza vilipoanza tarehe 7 Oktoba 2023.
Mwezi Julai mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitangaza kuwa ukaliaji wa muda mrefu wa Israel katika maeneo ya Palestina ni kinyume cha sheria, na kuitaka Israel kuondoa walowezi wake wote haramu katika Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa al-Quds (Jerusalem).