Vipigo vya Hizbullah vimeitia Israel hasara ya shekeli bilioni 9
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123182-vipigo_vya_hizbullah_vimeitia_israel_hasara_ya_shekeli_bilioni_9
Afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel amefichua kuwa, hasara iliyopatikana vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kutokana na vipigo vya Hizbullah wakati wa vita vya hivi karibuni inakadiriwa kuwa ni karibu shekeli bilioni 9 sawa na dola 2,515,582,638.
(last modified 2025-02-25T02:30:45+00:00 )
Feb 25, 2025 02:30 UTC
  • Vipigo vya Hizbullah vimeitia Israel hasara ya shekeli bilioni 9

Afisa mmoja wa utawala wa Kizayuni wa Israel amefichua kuwa, hasara iliyopatikana vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel, kutokana na vipigo vya Hizbullah wakati wa vita vya hivi karibuni inakadiriwa kuwa ni karibu shekeli bilioni 9 sawa na dola 2,515,582,638.

Tovuti ya habari ya Kanali 14 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni wa Israel imemnukuu Mickey Levy, mkuu wa kamati iliyoundwa na Israel kutathmini hasara zilizosababishwa na vita vya hivi karibuni vikiwemo vipigo vikali vya Hizbullah katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni akisema: "Wakazi wa kaskazini wanatakiwa kurejea majumbani na kwenye mashambani yao, na wanafunzi wanatakiwa kwenda maskulini, lakini hadi leo bado hatujalisikia baraza la mawaziri la Israel likisema limejitayarisha vipi kwa ajili ya mambo hayo."

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, wakuu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni wamekuwa wakipiga kelele mara kwa mara kwamba baraza la mawaziri la Israel halina uwezo wa kufanya chochote cha kuwawezesha wakazi wa kaskazini kurejea kwenye maisha yao ya kawaida baada ya vipigo vya Hizbullah na hasara za vita vya hivi karibuni. Bado walowezi wa Kizayuni wanaendelea kuishi kwenye hofu na kihoro cha vita. Topvuti hiyo ya kanali ya 14 ya televisheni ya Israel vilevile imesema kuwa, mwaka 2018, baraza la mawaziri la Israel lilitoa agizo la kutengwa shekeli bilioni 5 za kuyalinda maeneo ya kaskazini na kuboresha mazingira ya kujilinda na matukio mbalimbali lakini hadi hivi sasa ni shekeli milioni 100 tu ndizo zilizotumika. Ze'ev Elkin, waziri wa Israel anayehusika na masuala ya ardhi za kaskazini mwa Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni amewasilisha ripoti ya kina kuhusu hali na mazingira ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko kaskazini akisema: "Tulilazimika kuhama miji 43 na kukimbilia mbali na mpaka na Lebanon, miji hii ina wakazi 64,745."