Kadi nyingine nyekundu yatolewa kwa Israel; mara hii ni nchini Malaysia
Mashabiki wa soka wa Malaysia wamejiunga na kampeni ya 'Show Israel Red Card' yaani "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" katika uuwanja wa soka ili kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina.
Kampeni hii ya kuunga mkono Palestina dhidi ya Israel katika soka hadi sasa imetekelezwa katika nchi 30 duniani na watazamaji wa vilabu 72 wameipatia Israel kadi nyekundu.
Kampeni ya "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" ilianza hiivi karibuni wakati mashabiki wa timu ya soka ya Celtic ya Scotland walipolaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina na Lebanon katika mechi ya mkondo wa kwanza ya hatua ya mtoano ya UEFA Champions League dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani iliyochezwa siku ya Jumatano tarehe 12 Februari.
Mashabiki wa timu ya Celtic, maarufu kama Green Brigade waliongoza maandamano makubwa wakiwa na bango lililosema "Show Israel The Red Card," likizitaka UEFA na FIFA kuchukua hatua dhidi ya Israel katika mashindano hayo.
Hivi majuzi mashabiki wa klabu ya Osasuna ya Uhispania walitoa wito wa kukomeshwa uhalifu wa utawala wa Israel huko Palestina katika mechi na mpira wa miguu iliyofanyika kati ya timu hiyo dhidi ya Real Madrid.
Mashabiki wa Osasuna waliinua bango lenye maandishi: "Ionyeshe Israel Kadi Nyekundu" wakati wa mechi ya soka ya timu hiyo dhidi ya Real Madrid. Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, idadi kubwa ya mashabiki wa soka pia walifika kwenye uwanja huo wakiwa na bendera za Palestina.