Euro-Med Human Rights Monitor: Israel inatumia mateso kama silaha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i123342-euro_med_human_rights_monitor_israel_inatumia_mateso_kama_silaha
Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Mediterranean Human Rights Monitor limeeleza mshtuko wake mkubwa kutokana na hali mbaya ya kiafya na kisaikolojia ya mahabusi wa Kipalestina walioachiwa huru katika awamu ya saba ya utekelezaji wa makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Hamas na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2025-03-01T00:19:21+00:00 )
Mar 01, 2025 00:19 UTC
  • Euro-Med Human Rights Monitor: Israel inatumia mateso kama silaha

Shirika la kutetea haki za binadamu la Euro-Mediterranean Human Rights Monitor limeeleza mshtuko wake mkubwa kutokana na hali mbaya ya kiafya na kisaikolojia ya mahabusi wa Kipalestina walioachiwa huru katika awamu ya saba ya utekelezaji wa makubaliano ya kubadilishana mateka kati ya Hamas na utawala haramu wa Israel.

Euro-Med Human Rights Monitor imesema katika taarifa yake kwamba athari za mateso zinaonekana wazi kwenye miili iliyodhoofika ya mahabusi wa Kipalestina walioachiliwa, hali inayoakisi ukubwa wa uhalifu wa kimfumo na unyanyasaji wa kinyama waliokuwa wakifanyiwa ndani ya jela za Israel.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeongeza kuwa, Israel inaendelea kutumia mateso kama silaha ya kuwatia hofu na kuwanyanyasa mateka na mahabusu hadi dakika za mwisho za kuwekwa kizuizini, na kubainisha kwamba mateso ya kikatili na kupuuzwa kwa makusudi matibabu kumefikia viwango vya kustaajabisha vinavyokanyaga mipaka yote ya kimaadili na kisheria.

Taarifa ya Euro-Med Human Rights Monitor imesema kuwa timu ya uwanjani ya shirika hilo imeshuhudia majeraha makubwa miongoni mwa mahabusi wa Kipalestina walioachiliwa, ikiwa ni pamoja na kukatwa miguu na mikono, uvimbe mkubwa uliotokana na mateso, udhaifu mkubwa na uchovu. 

Mahabusi wa Palestina aliyekatwa mguu ndani ya jela ya Israel

Imeeleza kuwa baadhi ya mahabusi hao hawakuweza kutembea isipokuwa kwa msaada wa watu wengine, huku wengine wakihitaji huduma ya haraka wa matibabu kutokana na kuzorota kwa afya zao.

Euro-Med Human Rights Monitor imesisitiza kuwa kuna taarifa za kuaminika zinazoonyesha kuwa makumi ya mahabusu wa Kipalestina wameuawa ndani ya magereza ya Israel.

Baadhi ya Wapalestina Waliuawa kwenye jela za Israel

Shirika hilo limetoa wito wa kuwepo mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Israel ili isitishe aina zote za kuweka watu kizuizini kiholela, likitoa wito kwa nchi husika kuunga mkono kazi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kuchunguza jinai zinazofanywa dhidi ya mahabusu wa Kipalestina walioko katika jela za Israel.