Yemen yaitaka Riyadh ijifunze kutokana na hatma ya Zelensky
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amewaonya maafisa wa Saudi Arabia na kuwataka wapate somo na ibra kutokana na jinsi Marekani ilivyomfanyia Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, na kuwaonya dhidi ya kuitegemea kipofu Washington.
Mohammed Farah, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen ametoa indhari kali kwa viongozi wa Saudia, akiwataka kutafakari matukio ya hivi karibuni katika Ikulu ya White House, ambapo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alidhalilishwa.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X, Farah amezihutubu moja kwa moja mamlaka za Saudia akisema, "Je, uliona jinsi Marekani ilivyomfanyia mshirika wake mwaminifu zaidi katika Ulaya Mashariki, shakhsia wa Kiyahudi kama Zelensky? Je, walimtelekeza kwa urahisi kiasi gani? Una uhakika gani kwamba utajiri wako, uliowekwa kwenye benki za Marekani, utabaki salama?"
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Ansarullah ya Yemen amewasaili Wasaudia, je wana uhakika gani kwamba Wamarekani hawatawapa kisogo na kukemea matendo yao yote, kama walivyoifanya Ukraine?
Farah amesisitiza kwamba, iwapo Washington inaweza kuamiliana na washirika wake wa karibu kwa dharau na idhilali kama hiyo, hakuna chembe ya shaka kwamba mtazamo wake kwa ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu utakuuwa mbaya zaidi.
Matamshi ya Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen yanakuja wakati huu ambapo kumeshuhudiwa maendeleo ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya Saudi Arabia na Marekani.
Mwishoni mwa Januari mwaka huu, Rais Donald Trump alitoa wito kwa Saudi Arabia kuongeza kiwango cha uwekezaji wake nchini Marekani hadi dola trilioni moja.
Trump alisema hayo katika hotuba yake kwa njia ya video kwenye mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia huko Davos, Uswisi na kufichua kwamba, Riyadh inapanga kuwekeza dola bilioni 600 katika uchumi wa Marekani, lakini amesisitiza kuwa pesa hizo hazitoshi na inapasa kufikia dola trilioni moja.