Hizbullah: Muqawama uliilazimisha Israel kukubali usitishaji vita
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Hizbullah amesema Israel ilikubali kusitisha mapigano na Lebanon baada ya kupata vipigo vikali kutoka kwa wapiganaji shupavu wa Muqawama.
Akizungumza katika mahojiano maalum na kanali ya televisheni ya Al-Manar ya Lebanon Jumapili, Sheikh Naim Qassem amesema hatua ya Muqawama ya kushambulia makazi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu ilionyesha uwezo wake wa kufikia ndani kabisa hadi kwenye moyo wa utawala huo ghasibu.
Amesema wakati wa vita na Israel, Hizbullah ililenga tu kambi za kijeshi za utawala huo, licha ya kuwa na uwezo wa kushambulia popote katika ardhi hizo za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Sheikh Qassem amesisitiza Hizbullah kamwe haitaacha kufungamana na Muqawama dhidi ya Israel. "Watu wa Muqawama ndio watukufu na wenye heshima zaidi. Sasa, ninaelewa zaidi kwamba uhusiano kati ya (Shahidi) Sayyid (Hassan) Nasrullah na watu hauelezeki kwa maneno,” ameongeza.
“Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Nasrullah, tulikuwa na uratibu na Sayyid Hashem Safieddine, na tukakubaliana kuahirisha mazishi ili kuwalinda watu. Kadiri muda ulivyopita, hali hiyo ililazimu ucheleweshaji zaidi. Idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura haikuwa na kifani,” amesema.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Hizbullah ameeleza kuwa, "Nilihisi kwamba watu walikuwa wakitangaza, 'Tunabakia kuwa waaminifu kwako, Sayyid Nasrullah.' Muqawama sio hali tu, bali ni imani iliyokita mizizi na iliyokumbatiwa na wanaume na wanawake, vijana kwa wazee."
Kadhalika Sheikh Naim Qassem amezishukuru na kuzipongeza Iran na Iraq kwa kushiriki kwa wingi katika mazishi makubwa ya hivi karibuni ya Shahidi Nasrullah mjini Beirut.