Mjumbe wa UN asema mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Syria lazima yakome ‘mara moja’
(last modified Sun, 04 May 2025 02:26:13 GMT )
May 04, 2025 02:26 UTC
  • Mjumbe wa UN asema mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Syria lazima yakome ‘mara moja’

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Geir Pedersen, amelaani vikali ukiukaji unaozidi kuongezeka wa mamlaka ya Syria unaofanywa na utawala wa Israel, akisema utawala huo ghasibu lazima usitishe mashambulizi yake ya anga “mara moja.”

Pedersen amesema kupitia chapisho katika mtandano wa X kwamba: “Ninalaani vikali ukiukaji unaoendelea na unaoongezeka wa mamlaka ya Syria unaofanywa na Israel, ikiwa ni pamoja na mashambulizi mengi ya anga mjini Damascus na miji mingine.”

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameitaka Israel “iheshimu sheria za kimataifa na mamlaka, umoja, ukamilifu wa ardhi na uhuru wa Syria.” Amesema mashambulizi ya anga lazima yakome mara moja na kwamba Israel lazima iachane na “kuhatarisha maisha ya raia wa Syria.”

Utawala wa Israel ulitekeleza karibu mashambulizi 20 ya anga nchini Syria mwishoni mwa Ijumaa, jambo ambalo watawala wapya wa nchi hiyo ya Kiarabu wamelilaani na kulitaja kama “ongezeko hatari la mvutano.”

Mashambulizi ya Israel yalilenga maeneo karibu na mji mkuu, Damascus, na magharibi, katika maeneo ya Latakia na Hama, pamoja na Daraa kusini.

Kkwa uchache, raia mmoja aliuwawa katika kitongoji cha Damascus, na wengine wanne walijeruhiwa karibu na Hama. Wimbi hili jipya la mashambulizi ya anga ya Israel limekuja saa chache baada ya ndege za kivita za Israel kushambulia karibu na ikulu ya rais wa Syria mjini Damascus.

Watawala wa Israel pia wamedai kuwa mashambulizi hayo ni jaribio la kulinda walio wachache wa madhehebu ya Druze nchini Syria, ambao wamekuwa wakipambana na wanamgambo wanaoungwa mkono na kundi linaoltawala Syria ya Hay’at Tahrir al-Sham-led (HTS) katika wimbi jipya la vurugu za kimadhehebu, ambazo zimeacha watu kadhaa wakiwa wamekufa kusini mwa Damascus.

Jumamosi, Tume Huru ya Kimataifa ya Uchunguzi juu ya Syria ya Umoja wa Mataifa ilikanusha madai hayo ya Israel. Tume hiyo imesisitiza kuwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria yanatishia kuleta hali ya kutokua na utulivu nchini humo na ni jaribio la kugawa jamii nchi hiyo ya Kiarabu.

Taarifa hiyo ilibainisha kwamba: “Mashambulizi ya anga ya Israel na vitisho vya kuingilia kijeshi zaidi—wakati Israel ikiendelea kupanua ukaliaji wake wa eneo la milima ya Golan ya Syria na kujaribu kugawa jamii mbalimbali za Syria—yanahatarisha kuikosesha Syria utulivu zaidi.”