Yemen Yapiga marufuku usafirishaji wa mafuta ghafi ya Marekani kupitia Bahari Nyekundu
(last modified Sun, 04 May 2025 02:28:17 GMT )
May 04, 2025 02:28 UTC
  • Yemen Yapiga marufuku usafirishaji wa mafuta ghafi ya Marekani kupitia Bahari Nyekundu

Serikali ya Yemen imetangaza marufuku ya jumla dhidi ya mafuta ghafi ya Marekani, kama jibu kwa mashambulizi yanayoendelea ya Washington kwenye ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu, pamoja na mashambulizi yanayolenga raia na miundombinu ya kiraia.

Kituo cha Kuratibu Operesheni za Kibinadamu cha Yemen (HOCC) kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Jumamosi kikisema kuwa vikwazo dhidi ya Marekani vitaanza kutekelezwa Mei 17.

Mkurugenzi Mtendaji wa HOCC amesema marufuku hiyo imewekwa kuwa “adui wa Kimarekani” anayeendelea kufanya mashambulizi katika majimbo mbalimbali ya Yemen, akilenga raia na vituo vya kiraia, jambo lililosababisha vifo na majeruhi kwa mamia ya watu, wakiwemo wanawake na watoto.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Kama ambavyo adui wa Kimarekani alivyolenga bandari ya mafuta ya Ras Issa katika jimbo la al-Hudaydah mnamo Aprili 17, 2025, akishambulia miundombinu ya kiraia na wafanyakazi katika uhalifu wa kutisha unaotambuliwa kama moja ya mauaji ya kinyama dhidi ya binadamu, katika jaribio la kuzingira watu wa Yemen, Jamhuri ya Yemen ina haki ya kujibu uhalifu, mauaji ya kimbari, na uhalifu wa kivita unaofanywa na adui wa Kimarekani dhidi ya watu wa Yemen.”

“Hivyo basi, uamuzi umetolewa wa kupiga marufuku usafirishaji, uhamishaji, upakiaji, ununuzi, au uuzaji wa mafuta ghafi ya Marekani, iwe moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.”

Mkuu wa HOCC ameonya kuwa kampuni zitakazokiuka marufuku hiyo mpya ya usafirishaji mafuta zitawekwa kwenye orodha ya wavamizi dhidi ya Yemen, akisema meli zinazomilikiwa au kuendeshwa na kampuni hizo pia zitazuiwa kupita katika maji muhimu ya kikanda, ikiwemo Bahari Nyekundu, Mlango wa Bahari wa Bab al-Mandab, Ghuba ya Aden, Bahari ya Arabu na Bahari ya Hindi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kutakuwa na misamaha kwa madhumuni ya kibinadamu au kwa nchi na kampuni zinazopinga sera za Marekani, endapo zitatuma ombi rasmi kwa serikali ya Yemen.

Tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza, vikosi vya jeshi la Yemen vimeendesha oparesheni nyingi kuunga mkono Wapalestina wanaokumbwa na vita, vikishambulia ngome za kijeshi na kiuchumi za utawala wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, pamoja na kulenga meli za Israel au meli zinazoelekea bandari za maeneo hayo yaliyokaliwa kwa mabavu.

Kwa kuunga mkono Israel, Marekani ilitangaza kuunda kikosi cha majini mwezi Desemba 2023 ili kulinda meli zinazokwenda kwenye maeneo yanayokaliwa na Israel kupitia Bahari Nyekundu.

Vikosi vya Yemen vilijibu kwa kuongeza mashambulizi yao dhidi ya malengo ya kimkakati na nyeti ya Israel na Marekani, ikiwemo meli za kivita za Marekani zilizoko pwani ya Yemen.