Israeli inaiangamiza Gaza kwa njaa huku dunia ikinyamaza: Watoto 290,000 ‘katika hatari ya kifo’
Karibu watoto 290,000 wa Kipalestina wako “katika hatari ya kifo” Gaza huku Israel ikiendelea kutumia njaa kama silaha ya vita, maafisa wa Palestina wanasema.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema katika taarifa siku ya Jumapili kwamba zaidi ya watoto 70,000 wamelazwa hospitalini kutokana na utapiamlo mkali, na jamii ya kimataifa inaendeleza “ukimya wa aibu” kuhusu uhalifu huu.
“Chini ya mzingiro huu wa kimfumo,” ilisema taarifa, “zaidi ya watoto 3,500 walio chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na kifo cha karibu kutokana na njaa, huku takriban watoto 290,000 wakiwa kwenye ukingo wa kifo.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utawala wa Israel unaendelea kuzuia kuingizwa kwa maziwa ya watoto, virutubishi na aina zote za misaada ya kibinadamu katika ukanda huo wa pwani.
“Wakati ambapo watoto milioni 1.1 kila siku wanakosa mahitaji ya chini kabisa ya lishe kwa ajili ya kuishi, uhalifu huu unatekelezwa na utawala ghasibu wa ‘Israel’ kwa kutumia njaa kama silaha, huku dunia ikinyamaza kwa aibu.”
Kundi la utetezi wa haki za watoto la Oxfam limeonya kwamba hali ya kibinadamu inatarajiwa “kuzorota” zaidi Gaza.
Mahmoud Alsaqqa, kiongozi wa usalama wa chakula na maisha ya watu wa Oxfam huko Gaza, alisema, “Tumekuwa tukitoa onyo mara kwa mara kwamba hatua hii itasababisha madhara makubwa na yasiyoweza kurekebishwa, hasa kwa makundi yaliyo hatarini — watoto, wazee na wanawake.”
Alisema, “Dunia nzima, kwa bahati mbaya, inachangia au kushiriki katika kuwaangamiza watoto wa Ukanda wa Gaza kwa njaa.”
“Bila kuchukua hatua yoyote, kwa bahati mbaya wote wanakuwa washirika,” Alsaqqa alieleza.
Alsaqqa alisema jumuiya ya kimataifa ina “chaguo: aidha kuendelea kutazama tu hofu, picha na taswira zinazoibuka kutoka Gaza, au kuchukua hatua.”
Kwa miezi miwili sasa, Israel imezuia kuingia kwa dawa, mafuta na misaada ya chakula Gaza. Mashirika ya misaada yameonya mara kwa mara kwamba juhudi za kibinadamu Gaza ziko kwenye ukingo wa “kuporomoka kabisa.”