Hamas yakubali kumwachilia huru mateka Mmarekani-Muisraeli
(last modified Mon, 12 May 2025 05:51:35 GMT )
May 12, 2025 05:51 UTC
  • Hamas yakubali kumwachilia huru mateka Mmarekani-Muisraeli

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kuwa imekubali kumwachilia huru mateka Mmarekani-Muisraeli anayeshikiliwa huko Ghaza, baada ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Marekani kuhusu kusitishwa mapigano katika ukanda wa Ghaza uliozingirwa kila upande na Wazayuni.

"Mwanajeshi wa Israel, Edan Alexander, raia wa Marekani, ataachiliwa huru kama sehemu ya juhudi za kusitisha mapigano huko Ghaza," imesema taarifa ya Hamas ya jana Jumapili. 

Kiongozi wa Hamas huko Ghaza amesema kwamba Edan Alexander ataachiliwa huru kama hatua ya kwanza kuelekea usitishaji vita, kufunguliwa vivuko vya Ghaza na kufikishwa misaada ya kibinadamu. Khalil al-Hayya ameongeza kuwa, uamuzi huo umefuatia mawasiliano baina ya HAMAS na Marekani katika siku chache zilizopita mjini Doha Qatar. Amesema kuwa harakati ya HAMAS imeonesha nia yake njema wakati huu ambapo mazungumzo hayo yanaendelea.

Pia ametangaza kwamba HAMAS iko tayari kuanza mazungumzo ya kina ya kufikia makubaliano ya kumaliza vita kikamilifu na kubadilishana mateka na kwamba matumizi yoyote ya nguvu za kijeshi hayawezi kupelekea kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa huko Ghaza. 

Wakati huo huo, uchunguzi mpya unaonesha kuwa watu wasiopungua 109,000 wameuawa shahidi tangu Israel ilipoanzisha mauaji ya kimbari kwenye Ukanda wa Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023. Uchunguzi huo uliochapishwa na gazeti la The Lancet umepitia rekodi za hospitali, taarifa za vifo vya raia mtandaoni, na orodha iliyokusanywa kwa kujitegemea kwenye kumbukumbu za mitandao ya kijamii na matangazo ya vifo. Kwa kulinganisha orodha hizo tatu, watafiti wamehitimisha kuwa idadi ya watu waliouawa huko Ghaza ni kubwa zaidi ya ile iliyoripotiwa rasmi na mamlaka husika katika ukanda huo.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, Marekani imeutaka utawala wa Kizayuni usifanye shambulio lolote la kushtukiza dhidi ya Ghaza katika kipindi hiki ambacho Donald Trump anakaribia kulitembelea eneo la Asia Magharibi.