Kwa nini utawala wa Kizayuni ni utawala wa mauaji ya kizazi?
Sisitizo la Israel la kuendeleza vita Gaza katika mwezi wake wa ishirini na kuendelea kuwaua kwa umati wakazi wa ukanda huo hususan wanawake na watoto si tu kwamba kumeibua mijadala ya upinzani na kulaaniwa kimataifa kitendo hicho, bali hata nchi za Ulaya zimekuwa zikiukosoa utawala huo ghasibu kwa hatua zake hizo za kikatili.
Kuhusiana na hilo, Pedro Sanchez Waziri Mkuu wa Uhispania katika taarifa yake kwenye Bunge la nchi hiyo amesema, utawala wa Kizayuni ni utawala wa mauaji ya kimbari na kuwa nchi hiyo ina haki ya kukata nao uhusiano wa kibiashara.
Femke Halsema Meya wa Amsterdam pia awali alitoa wito kwa serikali ya Uholanzi ichukue msimamo thabiti dhidi ya uharibifu, njaa, na mauaji ya kikatili yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza, akisisitiza kwamba Ulaya lazima iwaunge mkono Wapalestina. Akinukuu ripoti kutoka Taasisi ya Kitaifa ya Mafunzo ya Usalama ya Uholanzi na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, Halsema amesema: 'Ni jambo la busara kuzungumzia ghasia za mauaji ya halaiki huko Gaza, na ni wakati wa kuweka kando tofauti zetu za kisiasa na kuzingatia kuokoa maisha ya binadamu." Meya huyo wa Amsterdam pia ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za kivitendo kutoka kwa serikali ya Uholanzi kuhusiana na suala hilo na kuongeza kuwa: "Suala la serikali kutoa tamko tu kuhusu haja ya kusitishwa ghasia huko Gaza bila kuchukua hatua za kivitendo katika uwanja huo halina maana."
Kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023, takriban watu 53,000 wameuawa kinyama huku idadi ya wale waliojeruhiwa katika mashambulizi hayo ikifikia takriban watu 120,000. Maelfu ya wengine bado hawajulikani walipo na wamekwama kwenye vifusi vya nyumba zilizoharibiwa katika ukanda huo. Njaa na ukosefu wa dawa na vifaa vingine vya matibabu pia vimeongeza vifo vya Wapalestina, haswa watoto na wajawazito. Kwa upande mwingine, shehena ya misaada ya chakula ya kimataifa inaendelea kuoza nyuma ya mipaka ya Gaza.

Tom Fletcher, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura amesema: "Israel inaweka kwa makusudi mazingira magumu na ya kinyama dhidi ya raia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu." Hakuna kilichoingia Gaza kwa zaidi ya wiki 10, si chakula, si dawa, si maji, si mahema. Mamia kwa maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuyahama makazi yao kwa mara nyingine tena, wakiwa wamebanwa kwenye maeneo madogo sana, huku asilimia 70 ya eneo la Gaza likiwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na askari wa Israel au yaliyo chini ya amri ya kuhamishwa wakazi wake." Amesisitiza kuwa zaidi ya Wapalestina milioni mbili katika Ukanda wa Gaza wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.
Siasa za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza zimeegemezwa kwenye msingi wa mauaji ya kimbari, ya makusudi na ya kila siku ya idadi kubwa ya watu wa ukanda huo hususan wanawake na watoto. Lengo la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika mauaji hayo ni kuwalazimisha watu wa Gaza waondoke katika eneo hilo, kwa kuendelea kutoa mashinikizo yasiyo na kikomo na vitendo vya ukatili, na pia kwa kutumia silaha ya njaa na njaa bandia huko Gaza.
Netanyahu anadhani kwamba kwa kutekeleza jinai hiyo na kuwafukuza Wapalestina kutoka Gaza, ataweza kufikia lengo lake la awali na aliloahidi kupitia operesheni za kijeshi la kuyaangamiza makundi ya muqawama ya Palestina hususan Hamas na hatimaye kuidhibiti kabisa Gaza. Jambo la kusikitisha ni kwamba Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, kama chombo chenye dhamana ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kiuhalisia zimeshindwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na Israel, kutokana na muundo wa kidhalimu wa baraza hilo na nguvu ya kura ya turufu ya nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Israel, yaani Marekani, Ufaransa na Uingereza.
Vitendo vya makusudi vya Israel katika mauaji ya kizazi dhidi ya watu wa Gaza vimepelekea taasisi za kimataifa hasa mahakama kuguswa na suala hili. Kuhusiana na hilo, tarehe 21 Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati ya kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wa Vita wa Israel Yoav Gallant kwa tuhuma za kutenda jinai za kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na kutumia njaa kama silaha ya vita. Uamuzi huo usio wa kawaida uliukasirisha sana utawala wa Kizayuni hasa kwa vile kufikia sasa umekuwa ukijaribu kupitia uungaji mkono wa Marekani, kuyaonyesha makundi ya muqawama wa Palestina hususan Hamas kuwa ni magaidi na wahalifu na hivyo kujidhihirisha kuwa muhanga wao.
Afrika Kusini pia iliwasilisha malalamiko kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki mnamo Desemba 29, 2023, dhidi ya Israel kwa kukiuka Mkataba wa Geneva wa 1948 unaopiga marufuku mauaji ya kimbari na kizazi dhidi ya Wapalestina. Katika uamuzi wa Januari 2024, mahakama hiyo ilitangaza kwamba Israel lazima ijiepushe na kitendo chochote kinachohusiana na mauaji hayo. Hii ni katika hali ambayo Israel imepuuza kabisa hukumu hiyo na kutokana na kuungwa mkono kikamilifu na Marekani na baadhi ya nchi nyingine kama Ujerumani, imeendelea kuwaua kinyama watu wa Gaza bila kujali lolote.