Walowezi wa Kizayuni wazidi kufanya uvamizi katika msikiti wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i12691-walowezi_wa_kizayuni_wazidi_kufanya_uvamizi_katika_msikiti_wa_al_aqswa
Walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena jana Ijumaa walifanya uvamizi dhidi ya msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa huko Quds Tukufu Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2016 23:14 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wazidi kufanya uvamizi katika msikiti wa al-Aqswa

Walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena jana Ijumaa walifanya uvamizi dhidi ya msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa huko Quds Tukufu Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Ripoti kutoka Palestina zinasema kuwa, walowezi wa Kizayuni Ijumaa ya jana waliendelea tena na vitendo vyao vya kuuvunjia heshima msikiti mtakatifu wa al-Aqswa, kibla cha kwanza cha Waislamu. 

Taarifa zaidi zinasema kuwa, walowezi hao wa Kizayuni wakisindikizwa na wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliingia katika uwanja wa msikiti huo kupitia upande wa Bal al-Maghariba.

Wanajeshi wa Israel wakielekea ndani ya Msikiti wa al-Aqswa

Kuingia katika eneo hilo takatifu walowezi hao kulipelekea kutokea mapigano kati yao na waumini waliokuwamo msikitini humo ambao walisikika wakipiga nara kupinga kuingia walowezi hao wa Kizayuni. Wazayuni hao baada ya kuingia msikiti hapo waliwatia mbaroni baadhi ya wahudumu wa msikiti huo.

Hii si mara ya kwanza kwa walowezi wa Kiyahudi kuuvamia msikiti huo mtakatifu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vinavyokinzana kabisa na heshima na utukufu wa msikiti huo.

Vurugu baina ya Wapalestina na askari wa Israel katika msikiti wa al-Aqswa

Hatua hizo za kuyavunjia heshima maeneo matakatifu huko Palestina zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hujuma hizo na ukandamizaji wa jeshi la Israel zimepelekea kutawanyika cheche za Intifadha mpya huko Palestina.

Vijana wa Kipalestina wakipambana kwa mawe na wanajeshi wa Israel

Itakumbukwa kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.