Ben Gvir alitaka jeshi la Israel litumie 'nguvu kamili' Gaza
Waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni wa Israel mwenye misimamo ya kufurutu ada, Itamar Ben Gvir ametoa wito wa kutumiwa "nguvu kamili" huko Gaza, baada ya madai ya uongo kwamba Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepinga pendekezo jipya la Marekani kuhusu usitishaji vita.
"Hakuna visingizio tena," Ben Gvir alisema kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Telegraph jana Ijumaa, akitoa mwito wa kutumiwa mbinu za kikatili zaidi dhidi ya wakazi wa Gaza.
Ben Gvir amesema, "Mkanganyiko, masumbuko na udhaifu lazima viishe. Tumepoteza fursa nyingi sana. Ni wakati wa kuingia kwa nguvu kamili bila kupepesa macho, kuharibu, na kuangamiza Hamas hadi wa (mwanachama wa) mwisho."
Waziri huyo wa Kizayuni ametoa mwito huo kwa madai kwamba Hamas imepinga pendekezo la Marekani. Hii ni katika hali ambayo, Hamas ilisema "uongozi wa kundi hilo la Muqawama unachunguza majibu ya pendekezo hilo kwa uwajibikaji kamili wa kitaifa."
Waziri huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada, mara kwa mara amekuwa akitoa matamshi ya kichochezi, mbali na kuuvunjia heshima msikiti wa al-Aqsa, huku akisindikizwa na polisi wa utawala ghasibu wa Israel.
Mauaji ya kimbari Gaza pamoja na vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.