Wanachama wa genge moja la kigaidi watiwa mbaroni Iraq
Idara ya Taifa ya Ujasusi ya Iraq imetangaza habari ya kutiwa mbaroni na kusambaritishwa mtandao wa uhalifu uliokuwa na nia ya kufanya operesheni za mauaji na kuvuruga usalama wa umma nchini humo.
Katika taarifa yake, Shirika la Ujasusi la Iraq limetangaza kuwa, kwa idhini ya Mahakama, limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa uhalifu ambao kutokana na taarifa zilizopatikana ulikusudia kufanya operesheni za mauaji na kuvuruga usalama wa raia kwenye maeneo tofauti ya Iraq.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa, maficho ya magaidi hao yalitibuliwa kwenye operesheni iliyofanyika kwa wakati mwafaka. Operesheni hiyo imefanyika kwa wakati mmoja katika mikoa kadhaa ya Iraq, ambapo maafisa usalama walivamia maficho ya magaidi hao na kuwatia mbaroni.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iraq, Idara ya Taifa ya Ujasusi ya nchi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kukabiliana na jaribio lolote la magenge yanayohatarisha usalama na kuiyumbisha Iraq kutokea ndani na nje ya nchi.
Shirika hilo limebainisha kuwa katika oparesheni ya kabla ya hii ya hivi sasa lilifanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi wanachama wa genge la uhalifu lililokusudia kuua na kuvuruga usalama wa umma nchini Iraq.
Shirika hilo limeeleza kuwa operesheni hiyo ilifanywa kwa kuzingatia taarifa sahihi za kijasusi na uchunguzi wa kina kuhusu jaribio la mauaji ya mwandishi wa habari mwezi Machi, na baada ya hapo vikosi vya shirika hilo vikafanikiwa kufika katika matawi ya genge hilo ambalo lilikuwa linaendeshwa na magaidi kutoka ndani na nje ya Iraq.