Kwa nini mashinikizo dhidi ya Netanyahu hayafanyi kazi?
(last modified Wed, 04 Jun 2025 11:02:21 GMT )
Jun 04, 2025 11:02 UTC
  • Kwa nini mashinikizo dhidi ya Netanyahu hayafanyi kazi?

Mauaji ya Wapalestina wanaoishi Gaza yanayofanywa na utawala wa Kizayuni yangali yanaendelea, huku nchi na jumuiya mbalimbali za kimataifa zikitoa wito wa kukomeshwa mauaji hayo mara moja.

Pamoja na hayo mashinikizo hayo ya kimataifa hadi sasa yameshindwa kumshurutisha Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel, asitishe jinai au kupunguza siasa zake za misimamo mikali na mauaji dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Maxime Prévot​​ , Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji amesema wazi kuhusu suala hili kwamba mashinikizo ya kimataifa kwa Israel hadi sasa hayajafanikiwa kwa sababu Marekani inamuunga mkono Netanyahu, uwe ni uungaji mkono wa kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au msaada wa moja kwa moja wa kifedha na silaha kwa utawala wa Israel. Suala hilo limeiweka Israel katika hali ambayo haiwezi kukosolewa wala kushinikizwa kupitia maonyo ya kimataifa.

Marekani imekuwa mshirika wa kimkakati wa Israel kwa miaka mingi, lakini wakati wa utawala wa Netanyahu, mahusiano haya yamefikia viwango visivyo vya kawaida vya mshikamano wa kisiasa; kwa kadiri kwamba Rais Donald Trump wa Marekani aliutambua mji mtakatifu wa Quds yaani Jerusalem kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha kwanza cha utawala wake.

Kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa Marekani mwaka uliopita, na licha ya jinai zote za kutisha zinazofanywa na Israel, Marekani sio tu imeendelea kuunga mkono sera za jinai za Netanyahu bali pia imepanua wigo wa uungaji mkono wake kwa utawala huo unaoua wanawake na watoto bila huruma. Katika hali hiyo, mbali na kuipatia Israel silaha za kila aina na kuunga mkono siasa za Wazayuni katika duru na taasisi za kimataifa, Marekani inaunga mkono kikamilifu sera mbili hatari za Israel ambazo ni za kuwafukuza Wapalestina kwa nguvu kutoka kwenye ardhi zao kutekeleza mauaji ya kimbari dhidi yao. Katika muktadha huo, Mike Huckabee, Balozi wa Marekani katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, alitoa wito wa kutengwa sehemu ya ardhi ya Ufaransa kwa ajili ya kuanzishwa taifa la Palestina, wito ambao unadhihirisha wazi kiburi na kutowajibika kwa viongozi wa Marekani kuhusu suala la Palestina. Msimamo huu sio tu kwamba unaonyesha kutowajibika Marekani kidiplomasia, lakini pia unaikejeli wazi jumuiya ya kimataifa na juhudi zake za kujaribu kutatua mgogoro wa sasa wa Palestina. Katika mazingira kama haya, ni wazi kwamba Netanyahu hawezi kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Ulaya au mashirika ya kimataifa.

Jinai za Israel Gaza

Uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa utawala wa kibaguzi wa Israel hauonekani tu katika kutumwa silaha na misaada isiyo na kikomo ya kifedha kwa utawala huo bali pia katika ngazi za kidiplomasia na kisheria. Marekani imetumia vibaya mara kwa mara kura yake ya turufu kwa ajili ya kupinga maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayoukosoa utawala wa Tel Aviv na hivyo kudumaza juhudi zozote za kimataifa za kikabiliana na jinai na uvamizi wa Israel katika Ukanda wa Gaza. Uungaji mkono huu usio na masharti wa Marekani kwa Wazayuni umewasilisha ujumbe wa wazi kwa Netanyahu na timu yake ya mauaji kwamba, wanaweza kuendelea na jinai na vitendo vyao vya ukatili na ugaidi dhidi ya Wapalestina bila kuwajibishwa kisheria katika ngazi za kimataifa.

Hata wakati baadhi ya wajumbe wa Congress na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanapotoa wito wa kusitishwa misaada ya silaha ya Marekani, hasa mabomu kwa utawala huo, Ikulu ya White House imekwepa suala hilo kwa kusisitiza juu ya kile kinachodaiwa kuwa "haki ya Israel kujilinda." Hii ni licha ya ripoti nyingi kutoka kwa mashirika ya kimataifa zinazoonyesha kuwa silaha hizo zinatumika moja kwa moja katika kuua raia na kulipua maeneo ya makazi, hospitali na shule.

Kuonyeshwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii picha za watoto na wanawake wa Gaza waliouawa kikatili, waliojeruhiwa na wanaoteseka kwa njaa, kumepelekea hata nchi za Ulaya zinazoiunga mkono Israel kulaani sera za jinai za utawala huo, na kwa namna fulani, kujaribu kujitenga na jinai hizo. Kwa mfano, Johann Wadephul, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani hivi karibuni alitangaza kuwa kutokana na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, nchi hiyo inatafakari upya mauzo ya silaha zake kwa Israel. Wakati Ujerumani siku zote imekuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa kijeshi na kidiplomasia wa Israel barani Ulaya, Ufaransa pia imejaribu kuchukua msimamo usioegemea upande wa Marekani kwa kufanya mkutano wa kimataifa wa kulitambua taifa la Palestina, suala ambalo limekabiliwa na maneno makali kutoka kwa balozi wa Marekani katika ardhi zinazoaliwa kwa mabavu.

Israel inaua bila huruma hata Wapalestina wanaojaribu kukimbilia misadaa ya chakula

Kwa uungaji mkono wake usio na masharti kwa Israel, Marekani imemweka Netanyahu kwenye eneo salama na kumshajiisha aendelee kufanya mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina huku akipuuza sheria, kanuni na matakwa yote ya kimataifa. Ni wazi kuwa hakuna mabadiliko yoyote ya kimsingi yatakayofanyika katika sera za mauaji za Israeli hadi pale Marekani na washirika wake wa Ulaya watakapoamua kutazama upya siasa zao za kutoa uungaji mkono usio na masharti kwa utawala wa kibaguzi wa Israel. Netanyahu anafahamu vizuri kuwa ulimwengu uko nyuma yake au umeamua kutazama tu jinai zake bila kumchukulia hatua za kisheria. Ni wazi kuwa mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Netanyahu yatafanikiwa tu pale yatakapokuwa na gharama kubwa za kisiasa na kiuchumi kwa Tel Aviv, jambo ambalo hadi sasa Marekani imelizuia kufikiwa.