Umoja wa Mataifa: Kuwanyima Wapalestina kupata chakula ni uhalifu wa kivita
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, akikosoa jinsi misaada inavyosambazwa katika Ukanda wa Gaza, ametangaza kuwa, kuwanyima raia kupata chakula huko Gaza kunaweza kuwa uhalifu wa kivita.
Akikosoa namna misaada inavyosambazwa, Volker Turk Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu amesema ni kinyume cha maadili kuwashambulia raia wa Gaza wanaojaribu kupata chakula kidogo.
Ameongeza kuwa: Utaratibu wa usambazaji wa misaada ambao Israel imeanzisha huko Gaza unatishia maisha ya binadamu na unakiuka viwango vya kimataifa vya misaada ya kibinadamu.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu ameongeza kuwa, kuwanyima raia kupata chakula na mahitaji ya kimsingi huko Gaza kunaweza kuzingatiwa kuwa uhalifu wa kivita.
Aidha amesema njaa, mauaji ya raia, uharibifu na kulazimika kuyahama makazi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi 20 ni uhalifu mkubwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Afisa huyo wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa ametaka uchunguzi wa haraka na usiopendelea upande wowote kuhusu mashambulizi dhidi ya raia wanaojaribu kupata msaada wa chakula huko Gaza na kusema kuwa, Wapalestina wanakabiliwa na machaguuo mawili machungu; Ama wanakufa njaa au wanauawa wakitafuta chakula.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kuwa zaidi ya watu milioni mbili katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na njaa kali, huku wengi wao wakikaribia kukumbwa na ukame na ukata wa ajabu.