Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah wasimama Arafa
Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu leo wamesimama katika uwanja wa Arafa kisimamo hicho kikiashiria kilele cha ibada tukufu ya Hijja.
Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na Mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.
Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SWT ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hijja na ameweka meza na karamu yake pembeni ya Jabalur Rahma.
Magharibi ya siku hii ya leo Mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hijja, kama kulala Muzdalifa, na kufanya amali ya Jamarat (kumpiga shetani kwa mawe saba).
Ibada ya Hija, ambayo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani, huwaleta pamoja Waislamu kutoka kila kona ya dunia kila mwaka huko Makkah Saudi Arabia.
Ibada tukufu ya Hija ni katika nguzo za Kiislamu. Ibada hii ya kisiasa na kimaanawi ni wajibu mara moja katika maisha ya Muislamu mwenye uwezo wa kifedha na kiafya.
Kwa mujibu wa mamlaka za Saudi Arabia, mahujaji karibu milioni mbili wanashiriki ibada ya Hija mwaka huu.
Mamlaka za Saudia zilisema zimeongeza tahadhari za usalama kwa mahujaji. Wamepanda maelfu ya miti na kuweka mamia ya viyoyozi katika sehemu mbali mbali za ibada ili kusaidia kupunguza halijoto kali huko.
Serikali ya Saudi Arabia pia imeweka marufuku ya kupeleka watoto walio chini ya umri wa miaka 12 na kuonya kuwa watu watakaojaribu kuhiji kinyume cha sheria bila kibali rasmi watakabiliwa na faini ya dola 5,000 na kupigwa marufuku kwa miaka 10 kuingia Saudi Arabia.